Na.Mwandishi Wetu – Dodoma
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amekutana na kufanya mazungumzo na Mtakwimu Mkuu Mpya wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, aliyefika kujitambulisha baada ya kuteuliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivi karibuni kuchukua nafasi ya aliyekuwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa, ambaye amestaafu rasmi utumishi wa Umma.
Kikao hicho kimefanyika Aprili 11,2025 katika Ofisi ya Waziri Mkuu iliyopo mtaa wa Reli jijini Dodoma.
Dkt. Yonazi amempongeza kwa uteuzi huo na kuahidi kuendeleza ushirikiano baina ya ofisi hizo huku akiwashukuru kwa kazi nzuri zinayofanywa na ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini.
“Ofisi hii inayoshughulikia masuala ya Takwimu ni muhimu sana katika nchi yetu, niwasihi mwendelee kuchapa kazi na kuwa wabunifu zaidi ili kuhakikisha Serikali inayafikia malengo yake nasi tutaendelea kushirikiana kuhakikisha tunaliletea Taifa maendeleo,” amesema Dkt.Yonazi

Akieleza namna Ofisi yake ilivyojipanga kutekeleza majukumu,Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Amina Msengwa amesema wapo tayari kufanya kazi huku wakihakikisha umma unapata taarifa zote muhimu zinazotakiwa kupitia program na mikakati iliyopo kwa kasi inayotakiwa.
Katika kikao hicho Mtakwimu Mkuu wa Serikali ameongozana na baadhi ya Watendaji wa Ofisi yake akiwemo Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi,Daniel Masolwa,Meneja wa Takwimu za Ajira, Bei na Mratibu wa mpango wa TSMP II Bw. James Mbongo, pamoja na Mratibu wa masuala ya Sensa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Adela Mpina.
More Stories
Chalamila:Dar ni salama,aelezea mafanikio na mipango ya maendeleo ya Mkoa
Ulaji vyakula vya aina moja,umri vyatajwa ongozeko la matatizo ya macho Mbeya
Kenya,Uganda zaanzisha mradi wa uendelezaji rasilimali za maji Angololo