Na Penina Malundo,Timesmajira
CHUO cha Kodi(ITA)kimetia saini ya makubaliano ya usimamizi wa kozi ya Uwakala wa Forodha Afrika Mashariki(EACFFPC) na Chama cha Mawakala wa Forodha (TAFFA) kwa lengo la kuendelea kutoa mafunzo ya forodha, kodi na Uwakala wa forodha kwa wadau wa Mamlaka ya Mapato na wananchi kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,wakati wa hafla ya kutiliana saini ya makubaliano hayo,Mkuu wa Chuo cha Kodi Profesa Isaya Jairo amesema Chuo chao kimekuwa mstari wa mbele katika ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika kuwajengea uwezo watumishi wa mamlaka za mapato kutokana na umahiri wake na kuwa na wataalam waliobobea katika masuala ya forodha na kodi.
Amesema anaamini kuwa ushirikiano huo,utaleta tija kwa wanachama wa TAFFA kwa kuwawezesha kufanya kazi kwa weledi na kisasa zaidi na kuhakikisha mapato yatokanayo na forodha yanaongezeka.
”Makubaliano haya ni fursa muhimu kwa mawakala wa forodha nchini kujiendeleza, hivyo TAFFA haina budi kuwahamisha wanachama wao kunufaika na mafunzo ya uwakala wa forodha kwani wakiwa na cheti cha Uwakala wa Forodha cha Afrika Mashariki kutoka ITA wanaweza kutumia.”Cheti hicho kufanya kazi za uwakala wa forodha mahali popote ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki na mahali popote duniani,”amesema.

Prof.Jairo amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki inahitaji mawakaala wa forodha wenye weledi ambao watapunguza changamoto zinazojitokeza katika tasnia ya uwakala wa forodha.
”Sisi Chuo cha Kodi tutatimiza wajibu wetu kuhakikisha TAFFA inaendesha Kozi ya EACFFPC kwa weledi na kwa kuzingatia misingi na matakwa ya Mtaala wa EACFFPC, wadhibiti wa elimu nchini ambao ni Wizara ya Elimu, Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) ili kulinda ubora wa kozi za ITA na taswira ya ITA pamoja na TRA kwa ujumla.

”Ni matumaini yetu kwamba ushirikiano huu utadumu na kupelekea kupatikana fursa nyingine za kushirikiana katika masuala mbalimbali ya forodna kama utafiti ili kuwa na mazingira bora ya utendaji kazi wa shughuli za forodha na tija kwa taifa kuzingatia kwamba ushirikiano huu haushii katika kusimamia kozi ya EACFFPC pekee bali pia programu nyingine za mafunzo katika nyanja za forodha na uwakala wa forodha kwa wanadau wa TAFFA,”amesema.
Kwa upande wake Rais wa TAFFA,Edward Urio amesema ushirikiano wanaoupata kutoka chuoni hapo ni mzuri kwani wao kama mawakala wa Forodha wako chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili waweze kutambulika na kuwa na leseni ya kufanya kazi za forodha.

Amesema TRA ni kiungo muhimu kwao ili kuhakikisha wanakuwa na watendaji wenye weledi na kukidhi viwango vya kukusanya kodi pamoja na kutengeneza wafanyakazi Bora watakaoweza kuingia kwenye soko la ushindani katika mipaka ya EAC na SADC kwani kwa sasa dunia inakwenda kuungana katika nyanja mbalimbali.
Mashirikiano yaliyosainiwa ni ya muda wa miaka mitano yakiwa na lengo la kuongeza ujuzi kwa mawakala wa Forodha na yatarejewa upya pale yatakapomalizika.
More Stories
The Desk and Chair yatoa vifaa saidizi kwa Masatu na mkewe
jengo la mama,mtoto la bilioni 6.5 lazinduliwa Mbulu
Dkt.Malasusa ataka hospitali ya Haydom kuombea wafadhili wanaoishika mkono