Fresha Kinasa TimesMajira Online Mara.
MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini,Prof. Sospeter Muhongo ameendesha Harambee ya kupata fedha na vifaa vya ujenzi wa shule ya Sekondari Kataryo ili kuhakikisha Wanafunzi wanaacha kutembea umbali mrefu kwenda masomoni.
Kijiji cha Kataryo ni moja ya vijiji vitatu vya Kata ya Tegeruka, ambapo Vijiji vingine ni vya Mayani na Tegeruka katika Jimbo la Musoma Vijijini Mkoani Mara.
Prof.Muhongo ameendesha harambee hiyo Machi 26, 2025 ambapo Wanakijiji walichangia mifuko 171 ya Saruji.Huku Mbunge Prof.Muhongo akichangia mifuko 200 ya suruji kwa ajili ya ujenzi huo.
Katika harambee hiyo, michango mingine iliyochangwa na Wanavijiji ni nondo 32, mchanga tripu moja, fedha Shilingi 150,000. Huku michango ya fedha kutoka kila kaya ikitarajiwa kuanza kukusanywa hivi karibuni.
Mbunge wa Jimbo hilo Prof.Muhongo amesema kuwa sababu zinazohamasisha ujenzi wa Kataryo Sekondari ni kwamba, Kijiji hicho kimeshiriki kujenga sekondari za Mugango (Kata jirani ya Mugango), na Tegeruka (Kata ya Tegeruka). Sekondari hizi mbili ziko mbali na Kijiji cha Kataryo kwa umbali wa kilomita kumi (Tegeruka Sekondari), na kumi na tano (Mugango Sekondari).
Pia ameongeza kuwa, sababu nyingine ni Mfumo mpya elimu ambao unamtaka kijana wa Tanzania kupata elimu ya Kidato cha Nne hivyo amewaomba wadau wote kujitokeza kuchangia ujenzi wa Sekondari ya Kijiji Cha Kataryo.
Kwa upande wao Wananchi wa Kijiji cha Kataryo akiwemo Majura Paulo amemshukuru Prof.Muhongo kwa kuendelea na harambee mbalimbali jimboni humo. Ambazo zimekuwa na matokeo makubwa katika kuimarisha sekta ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule, na maabara jimboni humo.
“Tutaendelea kuunga mkono juhudi za Mbunge wetu kuwezesha ujenzi wa Kataryo Sekondari.Shule nyingi amechangia ujenzi pia maabara zinazojengwa nguvu zake ni nyingi, lakini pia amefanikiwa kutuunganisha pamoja Wananchi katika suala la maendeleo bila kujali utofauti wa vyama.”amesema Jesca Abel.
More Stories
Vijana watahadharishwa kuelekea uchaguzi mkuu
Mkandarasi atakiwa kujenga haraka daraja la muda Bonyokwa
Rais Samia asisitiza amani nchini