March 31, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yaadhimisha siku ya hali ya hewa,kwa kuhakikisha uwekezaji wa  miundombinu ya hali ya hewa na usambazaji wa huduma zake. 

Na Penina Malundo,Timesmajira

MABADILIKO ya hali ya hewa na tabianchi yameendelea kuwa changamoto kubwa katika kufikia Malengo ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals-SDGs).

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, halijoto ya dunia imeendelea kuongezeka kutokana na ongezeko la gesi joto duniani ambapo kwa mujibu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), mwaka 2024 ulikuwa mwaka wa wenye joto zaidi katika historia ya upimaji wa taarifa hizi ambapo joto la wastani la dunia lilipanda kufikia takriban nyuzijoto 1.55°C juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda (1850-1900).

Kwa hali ilivyo mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwa ni pamoja na mvua kubwa, joto la juu ya wastani, upepo mkali, mafuriko, ukame, na vimbunga, yamekuwa makubwa zaidi na kuongezeka kwa idadi.

Lengo la 13 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG 13-katika kipengele cha kinachohusu Utekelezaji na Hatua dhidi ya mabadiliko ya Tabiachi) linazitaka Nchi Wanachama kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake.

Utekelezaji wa lengo hilo ni muhimu kwa maendeleo ya malengo mengine yote ya Maendeleo Endelevu ambapo kila mwaka  ifikapo Machi 23, kuadhimisha kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) tarehe hii mwaka 1950. 

Siku ambayo inaangazia mchango muhimu wa Taasisi za Hali ya Hewa katika usalama na ustawi wa jamii ambapo kulimbiu ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani mwaka 2025 ni ” Kwa Pamoja Tushughulikie Pengo la Utoaji wa Tahadhari.” Kaulimbiu inayosisitiza umuhimu wa juhudi za pamoja kuhakikisha kuwa Mifumo ya Tahadhari inamfikia kila mtu, hivyo kuboresha ustahimilivu wa jamii dhidi ya matukio ya hali mbaya ya hewa yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. 

Kaulimbiu hii pia inasisitiza kukusu utekelezaji wa mpango wa Umoja wa Mataifa wa tahadhari kwa wote (Early Warning for All-EW4All) ambao unalenga kuhakikisha kuwa kila mtu duniani anakuwa salama kupitia mifumo ya tahadhari dhidi ya matukio hatarishi ya hali ya hewa au maji ifikapo mwishoni mwa mwaka 2027

Tanzania kama Mwanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani na Umoja wa Mataifa pia inaadhimisha siku hiyo kwa kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na mapungufu katika utoaji wa tahadhari, ikiwa ni pamoja na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya hali ya hewa na kuwajengea uwezo wataalamu wa Mamlala ya Hali ya Hewa Nchini Tanzania.

Utoaji wa huduma za hali ya hewa na tahadhari kwa wakati na kwa usahihi ni muhimu sana katika kulinda maisha na mali dhidi ya matukio ya hali mbaya ya hewa kama vile mvua kubwa, mafuriko, ukame, joto kali, na vimbunga.

Akizungumzia maadhimisho ya siku hali ya hewa Duniani, Makame Mbarawa Waziri wa Uchukuzi  anasema Tanzania imeungana na mataifa mengine katika kusherekea siku hiyo ya hali ya hewa duniani ambapo imeweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na majanga ya hali mbaya ye hewa pamoja na mabadiliko ya tabianchi. 

“Serikali inapongeza kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Tanzania (TMA) katika utoaji wa huduma za hali ya hewa zilizoboreshwa sana, ikiwa ni pamoja na utoaji wa tahadhari wakati wa matukio ya hali mbaya ya hewa,”anasema.

“Serikali itaendelea kuimarisha huduma za hali ya hewa kwa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa zaidi na kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa TMA. 

Anasema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Serikali ya chini ya uongozi  Rais Samia Suluhu Hassan, katika kukabiliana na janga hili la mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na mapungufu katika utoaji wa tahadhari, ni pamoja na kuboresha huduma za hali ya hewa na utoaji wa tahadhari nchini. 

Anasema uboreshaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa ibara ya 59J ya Ilani ya Uchaguzi ya  Chama cha Mapinduzi (CCM), inayoitaka Serikali kuimarisha miundombinu ya hali ya hewa na ile ya utoaji wa tahadhari .

Mbawara anasema pia ni sehemu ya utekelezaji wa “Mfumo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma za Hali ya Hewa-(National Framework for Climate Services-NFCS) ambao unalenga kuimarisha utoaji na matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa kwa jamii.  

“Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya hali ya hewa na usambazaji wa huduma za hali ya hewa kwa jamii, ikiwa ni pamoja na ununuzi na uwekaji wa Rada za hali ya hewa, vituo vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe (Automatic Weather Stations) na Kompyuta kubwa na ya kisasa yenye uwezo mkubwa wa uchakataji wa data za hali ya hewa kwa ajili ya utoaji wa utabiri wa hali ya hewa.

” Kwa mujibu wa WMO, kila dola 1 ya Kimarekani inayowekezwa katika utoaji wa tahadhari inakadiriwa kurudisha faida dola 10 ambapo kwa baadhi ya maeneo mengine duniani, faida hizi zinaweza kuwa kubwa zaidi,”anasema.

Anasema Tanzania kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo imeendelea kuboresha miundombinu ya hali ya hewa nchini kupitia programu mbalimbali.

Akitaja moja ya programu hizo ni pamoka na utekelezaji unaoendelea wa mradi wa “Systematic Observations Financing Facility (SOFF)” wenye lengo la kuboresha miundombinu ya hali ya hewa nchini ambao utachangia kwa kuongeza vituo tisa  vipya vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe vya upimaji wa hali ya hewa usawa wa ardhi, vituo vinne vipya vya upimaji wa hali ya hewa ya anga za juu, na kuboresha vituo 18 vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe vya upimaji wa hali ya hewa usawa wa ardhi na kituo kimoja cha upimaji wa hali ya hewa wa anga za juu. 

“Uboreshaji huu utaongeza ufanisi wa kiutendaji wa TMA na hasa utoaji wa tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa nchini huku  kupunguza  athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

” Serikali imeweka na inatekeleza mipango mbalimbali ikiwemo kuhamasisha matumizi ya nishati safi. Kwa kuzingatia mahitaji ya huduma za tahadhari kutokana na kuongezeka kwa matukio makubwa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ambapo mabadiliko haya yanachagizwa na ongezeko la gesi joto kutokana na shughuli za binadamu, ikiwa ni pamoja na matumizi ya mafuta ya magari na mitambo kama chanzo cha nishati,”anasema.

Aidha anasema Rais Dkt.Samia anaendelea na  juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi, hasa katika nishati ya kupikia kama sehemu ya juhudi zake za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na kuboresha afya ya jamii. 

Anasema matumizi ya nishati safi ya kupikia yatachangia  katika malengo mapana ya maendeleo endelevu, uhifadhi wa mazingira, na ukuaji wa uchumi, lakini pia kupunguza uzalishaji wa gesijoto.  

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka TMA na Makamu  Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa na Tabianchi  (IPCC),Dkt.Ladislaus Changa anasema 

Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya hali ya hewa kwa lengo la kuboresha huduma za hali ya hewa na kuwezesha ustahimilivu dhidi ya majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa.

Anasema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, serikali imeongeza na kuboresha miundombinu ya hali ya hewa katika nyanja zote za utoaji wa huduma ya hali ya hewa ikiwemo ununuzi wa mitambo miwili 2 ya rada za hali ya hewa zilizofungwa katika mikoa ya Kigoma na Mbeya ili kuimarisha uangazi wa hali ya hewa, Vifaa vinavyotumika kuhakiki vifaa vingine vya hali ya hewa ili kuwa na upimaji sahihi wa taarifa za hali ya hewa, Vitambuzi vya radi na Kompyuta yenye uwezo mkubwa wa kuchakata taarifa za hali.

“Serikali imeendelea kuwekeza katika mafunzo kwa wataalamu wa hali ya hewa kwa lengo hilo hilo la kuboresha utabiri na huduma za hali ya hewa.

Juhudi hizi za Serikali zimesababisha kuongezeka kwa usahihi wa utabiri wa hali ya hewa hadi kufikia zaidi ya asilimia 88 kwa sasa.

“Usahihi huu wa utabiri wa hali ya hewa umefanya huduma zitolewazo na TMA kuwa za kuaminika zaidi, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kila siku za kijamii na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuokoa maisha na kulinda mali dhidi ya athari za hali mbaya ya hewa,”anasema.

Dkt.Chang’a anasema utoaji wa huduma za hali ya hewa na tahadhari kwa wakati na kwa usahihi ni muhimu sana katika kulinda maisha na mali zao dhidi ya matukio ya hali mbaya ya hewa kama vile mvua kubwa, mafuriko, ukame, joto kali, na vimbunga.

Anasema matumizi ya teknolojia za kisasa, zikiwemo zile za Setilaiti, Rada, Modeli za utabiri wa hali ya hewa, na vituo vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe, ni muhimu katika kuboresha na kuongeza usahihi wa utabiri wa hali ya hewa na ufuatiliaji wa hali ya hewa kwa wakati.

“Usambazaji wa taarifa za hali ya hewa zinazozalishwa na teknolojia hizi ili kuifikia jamii katika maeneo mengi hasa yale ambayo hayajafikiwa na huduma hizi kwa wakati na kwa gharama ndogo ni jambo muhimu sana kwa ulinzi wa maisha na mali na kuleta ufanisi katika kupanga na kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo katika sekta zote za kijamii na kiuchumi.

“Katika kushughulikia pengo la utoaji wa huduma za tahadhari nchini, TMA inatumia teknolojia za kisasa kama vile matumizi ya Akili Mnemba (AI), Matumizi ya modeli za kompyuta za kisasa (Machine Learning), na Uchambuzi wa Data nyingi kwa wakati mmoja (Big Data Analytics) kwa muktadha mzima wa kuboresha huduma za tahadhari za hali ya hewa ambazo ni muhimu sana katika utoaji wa maamuzi katika sekta mbalimbali na umma kwa ujumla,”anasema.