March 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujenzi Maabara za masomo ya sayansi waendelea Musoma Vijijini

Fresha Kinasa TimesMajira Online Mara.

Ili kuandaa wasomi na wataalamu mahiri wa nyanja mbalimbali watakaokuja kusaidia jamii na Taifa kwa siku za usoni,jimbo  la Musoma Vijijini lililopo Mkoa wa Mara  limejidhatiti kuhakikisha kila Sekondari jimboni humo inakuwa na maabara tatu za masomo ya sayansi yaani  Fizikia, Kemia na Bailojia.

Hiyo itasaidia wanafunzi kusoma masomo hayo kwa vitendo na kuongeza ufaulu wa masomo ya Sayansi.

Hayo yamesemwa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo kupitia taarifa yake ya Machi 17, 2025. “

Ambapo imesema Jimbo hilo lina mradi kabambe wa ujenzi wa maabara hizo tatu kwa kila Sekondari ya Kata.

“Wanavijiji na Viongozi wanashirikiana na Halmashauri yetu (Musoma DC), na Serikali Kuu kuchangia ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi kwenye Sekondari zetu za Kata.”amesema Prof. Muhongo.

Aidha ametaja malengo ya ujenzi wa maabara hizo za Sayansi kuwa  ni kuboresha ufundishaji, ujifunzaji, uelewa na ufaulu wa masomo ya sayansi kwa wanafunzi Jimboni humo.

“Uanzishwaji wa “High Schools” za masomo ya sayansi Jimboni mwetu,kwa sasa tunayo “High School” moja tu nayo ni ya masomo ya “arts”- Kasoma High School.Wizara imetoa kibali cha kufunguliwa “High Schools” mpya mbili za masomo ya sayansi, ambazo ni  Suguti na Mugango High,”amesema.

Akitaja idadi ya maabara za masomo ya sayansi ndani ya Jimbo hilo,amesema   Sekondari zenye maabara tatu ni  sita, zenye maabara mbili ni nane,zenye maabara moja ni nne na zisizo na maabara ni nane, huku Sekondari za Madhehebu ya Dini  Nyegina ni maabara mbili na Bwasi mbili.

Amesema Sekondari hizo nane zisizokuwa na maabara ni Bukwaya,Kata ya Nyegina,
Busambara kata ya Busambara,Ifulifu kata ya Ifulifu,Murangi kata ya Murangi,Mtiro kata ya Bukumi,Nyanja kata ya Bwasi,Seka kata ya Nyamrandirira na Tegeruka kata ya Tegeruka.

Prof.Muhongo ametoa wito kwa Wadau mbalimbali wa elimu kujitokeza kuchangia  ujenzi wa maabara tatu za masomo ya sayansi kwenye sekondari hizo nane pamoja na Sekondari nne zenye maabara moja  ambazo ni Bukima Kata ya Bukima,Dan Mapigano Memorial Sec kata ya  Bugoji,Mabuimerafuru kata ya Musanja na  Kasoma Kata ya Nyamrandirira

Kuhusu ujenzi wa Maabara tatu za masomo ya Sayansi  Mtiro  Sekondari Prof.  Muhongo amesema wachangiaji wa ujenzi wa maabara hizo tatu za masomo ya sayansi  za shule hiyo ya Kata ya Bukumi yenye Vijiji vya Buira, Bukumi, Buraga na Busekera ametaja kuwa ni wanavijiji,  Mbunge wa Jimbo, Mfuko wa Jimbo na Halmashauri ya (Musoma DC). 

Amesema,Sekondari ya Mtiro inakaribia kukamilisha vigezo vya kuanzishwa kwa “High School” ya masomo ya sayansi ambapo Maji ya bomba  yapo, Umeme upo, Bweni la wanafunzi lipo na Maabara zinajengwa.

Kwa upande wao wananchi wa Musoma Vijijini wamesema kuwa, masomo ya Sayansi ni muhimu kwa Maendeleo ya nchi kiuchumi, hivyo wanapongeza juhudi za Mbunge wa Jimbo hilo kwa juhudi zake za  kuhakikisha kila Sekondari inakuwa na maabara hizo Watoto wasome kwa vitendo.

“Sayasi ni maisha, ili Taifa lizidi kupiga  hatua, lazima tuwekeze kwa Vijana wasome Sayansi kwa ajili ya kuja kusaidia tafiti mbalimbali, kuvumbua mambo muhimu yatakayoleta tija kwa Jamii.  Ujenzi wa maabara hizi unafaida Sana  niiombe serikali, ikahikishe inatoa ajira kwa Walimu wa Sayansi  wasaidie kufundisha  Watoto wasome kwa vitendo. Tunamshukuru Mbunge wakati mwingine amekuwa akitoa fedha zake mfukoni kusaidia kuwalipa Walimu wa muda wa masomo hayo.”amesema Jefta Masato.