Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani itakayoenda sambamba na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa itakayofanyika Machi 21, 2025 Mkoani Njombe.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) katika kikao na Watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zilizo chini ya Wizara kilichofanyika leo Machi 18,2025 Mtumba jijini Dodoma.
“Maadhimisho ya mwaka huu yana lengo la kuhimiza, kuelimisha na kuhamasisha Watanzania juu ya umuhimu wa kulinda na kuhifadhi rasilimali za misitu nchini. Kauli Mbiu ya mwaka huu ni ‘‘Ongeza Thamani ya Mazao ya Misitu kwa Uendelevu wa Rasilimali kwa Kizazi Hiki na Kijacho’’ na Mgeni Rasmi wakati wa kilele atakuwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”Chana

Chana ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo na maono yake katika kuendeleza masuala ya misitu na uhifadhi hasa katika utalii.
“Katika uongozi wa Rais Samia tumeshuhudia sekta ya misitu ikiendelea kuimarika siku hadi siku hivyo ni wajibu wetu Watanzania kuhakikisha kwamba tunalinda misitu yetu isipate uharibifu wa aina yoyote” Chana amesema.

Amefafanua kuwa Maadhimisho hayo yatahusisha shughuli mbalimbali ikiwemo zoezi la upandaji miti katika Halmashauri zote za Mkoa wa Njombe, maonesho ya bidhaa na huduma za misitu, midahalo itakayohusisha wataalam na wadau wa misitu, maonesho ya vivutio mbalimbali vya kitalii ikiwemo Wanyamapori hai kama Simba na wanyama wengine.Maadhimisho hayo yanafanyika kwa kuzingatia maazimio yaliyotolewa na Bazara Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2012.
More Stories
Wasira atoa siku 14 mnunuzi wa kahawa kulipa zaidi ya milioni 600 za wakulima
Msigwa:Mradi wa barabara Kibaha- Chalinze-Morogoro haujafeli
Kapinga:Maeneo ya kijamii yamepewa kipaumbele kufikiwa na umeme