March 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mavunde aagiza mradi wa Kabanga Nickel kutekelezwa kwa wakati

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Serikali kupitia Wizara ya Madini imeiagiza Kampuni ya ya uchimbaji wa Madini ya Tembo Nickel Corporation LTD kuhakikisha inatekeleza kwa wakati mradi wa Kabanga Nickel Project ambao unalenga uchimbaji wa Madini ya Nikeli na usafishaji wa madini hayo hapa nchini.

Maagizo hayo yalitolewa Machi 17, 2025, Jijini Dodoma na Waziri wa Madini,Anthony Mavunde wakati wa wasilisho kuhusu maendeleo ya mradi wa Kabanga Nikeli lililowasilishwa na Kampuni ya Tembo Nickel Corporation ambapo amesisitiza mradi huo kutekelezwa kwa wakati ili kuchochea maendeleo ya Sekta ya Madini nchini.

“Mradi huu ni mradi mkubwa na muhimu sana kwa maendeleo ya Sekta ya Madini. Tutahakikisha masuala yote yaliyobaki yanakamilika kupitia Timu ya majadiliano ya Serikali na mwekezaji. Na kwa upande wa mwekezaji ni muhimu kuhakikisha anakamilisha masuala yote yaliyo upande wake ili shughuli za uendelezaji wa mradi wa mgodi zianze kwa uharaka“ Amesema Mavunde

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Life Zone Metals Chris Showalter amesisitiza kuhusu dhamira ya Kampuni hiyo kutekeleza uendelezaji wa mradi huo utakaohusisha shughuli za uchimbaji nikeli Wilayani Ngara, Mkoani Kagera na ujenzi wa kiwanda cha kusafisha madini hayo kitakachojengwa Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga.