March 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas Tanzania yafuturisha wateja wake Zanzibar

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online

KAMPUNI ya Yas Tanzania, imefanya hafla maalumu ya futari na wateja wake wa Zanzibar katika Hotel Verde, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 100 tangu mabadiliko rasmi ya chapa kutoka Tigo, TigoZantel na Tigo Pesa kwenda Yas na Mixx by Yas.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wakiongozwa na Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa, washirika wa kibiashara, wateja wa Yas & Mixx by Yas, na wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Idrissa Kitwana Mustafa ameipongeza Yas Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kukuza uchumi wa Zanzibar kupitia huduma za mawasiliano pamoja na huduma za kifedha kwa njia ya simu.

Vilevile, alitumia fursa hiyo kuishauri Kampuni ya Yas Tanzania kutuma jumbe za kuhamasisha amani kwa wateja wake kwakua mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi.

“Yas Tanzania imeendelea kuonyesha dhamira ya dhati katika kuwahudumia wateja wake na jamii ya Zanzibar kwa ujumla. Hata hivyo, kwa kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, naomba kampuni hii itumie majukwaa yake mbalimbali kuhamasisha amani, utulivu, na mshikamano miongoni mwa wananchi,” amesema Kitwana.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, Innocent Rwetabura, ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano wake katika kufanikisha mabadiliko ya chapa za Yas na Mixx by Yas, ambayo yameleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya mawasiliano nchini.

“Tunaposherehekea siku 100 za Yas na Mixx by Yas, tunajivunia kuwa tumeweza kuwa karibu zaidi na wateja wetu na kuwafungulia fursa nyingi za kidijitali. Katika kipindi hiki kifupi, tumepokea mapokezi chanya kutoka kwa wateja wetu.

“Tumeendelea kuwekeza katika teknolojia na huduma bora ili kuimarisha zaidi uzoefu wao,” amesema Rwetabura katika hotuba yake.

Afisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, Innocent Rwetabura akihutubia wageni waalikwa (hawapo pichani) katika hafla maalum ya Iftar iliyoandaliwa na Kampuni hiyo katika Hoteli ya Verde, Zanzibar hivi karibuni.

Rwetabura alieleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika siku 100 za Yas na Mixx by Yas, ikiwa ni pamoja na tuzo mbalimbali za umahiri.

Yas imepokea tuzo za kimataifa na kitaifa, ikiwemo kutoka kwa Ookla na TEHAMA Awards, pamoja na kutambuliwa na TRA kama mlipaji mkubwa wa kodi katika Ushuru wa Forodha.

Ushirikiano wa kimkakati, Yas imeanzisha ubia na taasisi mbalimbali kama Zanzibar Petroleum Limited (ZPL), DSE, na e-Government Agency Zanzibar (EGAZ) ili kuimarisha huduma zake kwa Watanzania.

Uwekezaji katika miundombinu: Kampuni imeongeza idadi ya minara yake nchini hadi kufikia zaidi ya 4,000 ili kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano na intaneti yenye kasi.

Kampeni ya “Magift ya Kugift”: Kupitia promosheni hii, zaidi ya Watanzania 1,300 wamenufaika kwa kupata zawadi zikiwemo magari mawili mapya, zawadi za fedha taslimu zenye thamani ya zaidi ya TZS milioni 840, na simu janja zaidi ya 540.

Rwetabura aliwashukuru wateja wa Zanzibar kwa kuendelea kuunga mkono Yas na Mixx by Yas, huku akisisitiza kuwa kampuni itaendelea kutoa huduma bora zinazokidhi mahitaji ya wateja wake.

“Zanzibar ni sehemu muhimu ya safari yetu ya kuwafungulia Watanzania fursa za kidijitali. Tunajivunia wateja waaminifu ambao wameendelea kuwa nasi katika mabadiliko haya makubwa. Ahadi yetu ni kuendelea kuboresha huduma zetu ili ziwe za viwango vya kimataifa,”.

Aliongeza kuwa, katika hitimisho la hafla hiyo, Yas Tanzania iliahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza uchumi wa visiwa hivyo kupitia huduma zake za kidijitali na mawasiliano.