March 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Daraja la mto Kagatende Suluhisho la Kudumu Utalii na Uhifadhi Serengeti

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

MWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Jenerali (Mst.) George Marwa Waitara ameiagiza Menejimenti ya TANAPA kuhakikisha kuwa ujenzi wa daraja la Mto Kogatende unakamilika kwa wakati na kwa ubora ili kuruhusu shughuli za uhifadhi na utalii kuendelea.

Jenerali Waitara ametoa maagizo hayo Machi 13, 2025, wakati Bodi ya wadhamini ya TANAPA, ilipotembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti ili kujionea eneo la daraja hilo ambalo halipitiki kutokana na uharibifu mkubwa uliotokana na mvua kubwa zilizonyesha mwaka 2020 na 2024.

“Ujenzi wa daraja ufanyike kwa wakati bila kikwazo chochote kwani ni muhimu sana kwa ustawi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti kiutalii na kiuhifadhi. Tunahitaji miundombinu imara katika hifadhi zetu ili shughuli za uhifadhi na utalii ziweze kufanyika vizuri.

“Ujenzi wa daraja hili ni suluhisho la kudumu na Menejimenti ihakikishe mradi huu unakamilika kwa wakati na kwa ubora ili liweze kupitika kwa kipindi chote cha mwaka,” amesema Waitara.

Naye, CPA Khadija Ramadhani, mjumbe wa Bodi ya Wadhamini TANAPA alisema kuna haja ya kuwa na daraja la juu kwa sababu hisitoria inaonyesha kwamba daraja hilo awali lilikuwa mita 5 limeendelea kupanuka hadi kufikia mita 126.

“Gharama za upanuzi zimekuwa zikiongezeka kila wakati hivyo kuna haja ya kujenga daraja la kudumu ili kuepuka gharama za matengezo ya mara kwa mara kwa menejimenti,” amesema CPA Khadija.

Akieleza historia ya daraja hilo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Stephano Msumi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, amesema awali daraja hilo lilikuwa la boksi (vented drift) ambalo lilikuwa likitumika wakati wa kiangazi tu kutokana na kuwa la chini.

“Daraja hili lilikuwa la boksi na lilikuwa chini hivyo kupitika wakati wa kiangazi tu. Hata hivyo limeendelea kuharibika kwa kiwango kikubwa kutokana na mvua zilizonyesha mwaka 2020 na 2024 ambapo kulikuwa na mvua kubwa sana,” amesema Kamishna Msumi.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Nuhu Daniel ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mendeleo ya Hifadhi amefafanua, mpaka sasa tayari uchambuzi wa taarifa za awali umeshafanyika ili kubainisha kina cha maji katika mto, hali ya udongo katika eneo la ujenzi wa daraja na historia ya ukubwa wa mafuriko katika mto huo kwa miaka 30 iliyopita ili kubainisha kimo cha daraja na kuwezesha usanifu wa michoro utakaokidhi viwango.

Amesema, kazi inayoendelea hivi sasa ni ukamilishaji wa usanifu wa kina na kuandaa michoro na nyaraka za zabuni ili kuanza taratibu za manunuzi ya mkandarasi.

“Tunaendelea kukamilisha usanifu wa kina kwa ajili ya maandalizi ya nyaraka za zabuni ya manunuzi ya mkandarasi yaweze kufanyika ili kuwezesha ujenzi kuanza.

“Ujenzi wa daraja hili unakwenda kubadilisha kabisa uendeshaji wa utalii upande wa Kaskazini ambapo waendesha utalii wataweza kutumia upande wa pili wa mto katika eneo la Lamai kiutalii hasa wakati msimu wa uvukaji wa nyumbu (Mara Crossing),” amesemaKamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Nuhu Daniel.

Mradi wa daraja la Kogatende lenye urefu wa mita 100 unatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Ujerumani kupitia benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) na utagharimu kiasi cha Euro milioni 2.2 sawa na kiasi cha takribani TZs bilioni 6.3.

Hata hivyo, mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi Novemba, 2025. Huo ni mwendelezo wa ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati nchi yetu na Serikali ya Jamhuri ya Ujerumani.

Bodi pia, ilitembelea miradi mingine inayoendelea kutekelezwa katika Hifadhi ya Taifa Serengeti ambayo ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Banagi – Lobo – lango la Kleins yenye urefu wa kilomita 72, barabara ya Golini – Naabi – Seronera yenye urefu wa kilomita 68 na ujenzi wa uwanja wa Golf “Serengeti National Park Golf Course” inayotekelezwa na kampuni tanzu ya TANAPA “TANAPA Investment Limited (TIL)” na ujenzi wa lango la Kleins unaotekelezwa na kampuni ya Stance Technic and Civil Engineers Limited.