March 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DAWASA:Upatikanaji huduma ya maji Dar asilimia 93

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam(DAWASA)imesema kwa sasa uwezo wa kuhifadhi maji umeongezeka kutoka lita 153,649,000 hadi lita 198,965,000 sawa na ongezeko la lita 45,316,000.

Hivyo imesaidia kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma ya majisafi kutoka wastani wa asilimia 89 hadi asilimia 93 na huduma ya usafi wa mazingira kutoka asilimia 25 hadi asilimia 45.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo Machi 11,2025 na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA,Mhandisi Mkama Bwire,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Amesema uwezo wa uzalishaji maji umeongezeka kutoka lita 520,000,000 kwa siku mpaka lita 534,600,000 kwa siku sawa na ongezeko la lita 14,600,000 kwa siku

Huku Mtandao wa usafirishaji na usambazaji maji ukiongezeka kutoka kilomita 4,690.7 hadi kilomita 7,206 sawa na ongezeko la kilomita 2,513.4

Mha.Bwire amesema mtandao wa majitaka umeongezeka kutoka kilomita 450 hadi kilomita 519.4 sawa na ongezeko la kilomita 69.4 na idadi ya maunganisho ya wateja wa majisafi imeongezeka kutoka 343,019 hadi 455,720 sawa na ongezeko la wateja 112,701.

Pamoja na mafanikio mengine DAWASA imesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kuanza kwa utekelezaji wa bwawa la Kidunda – Mkataba wenye thamani ya Sh bilioni 335.9, hadi sasa Sh bilioni 85.4 zimetolewa
na mradi umefikia asilimia 28

“Vilevile kutolewa kwa kibali cha kuanza maandalizi ya mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji ambapo utatosheleza mahitaji ya maji hadi mwaka 2050, utekelezaji wa kuandaa michoro ya
mwisho (detailed design) pamoja na kuandaa nyaraka za manunuzi (bidding documents) umefikia asilimia 8,”amesema Mha.Bwire.

Vilevile Mha.Bwire amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2021,DAWASA imeendelea na utekelezaji wa miradi zaidi ya 25 yenye thamani ya fedha za kitanzania Shilingi billioni 987.6.

Ambapo kati ya hizo bil.987.6,miradi yenye thamani ya bil. 232.9 imekamilika na inatoa huduma kwa wananchi.Huku miradi yenye thamani ya bil. 754.7 bado ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Aidha amesema miradi iliyopo katika mipango ya muda mfupi na mrefu yenye thamani ya Tsh Trilioni 3.1 imebuniwa na iko katika hatua mbalimbali za maandalizi.