March 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Biteko ataka wanawake kubeba ajenda ya Samia

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka wanawake kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia kwa kuibeba ajenda hiyo muhimu ambayo, Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa akiipa kipaumbele akiwa ndani na nje ya nchi.

Amesema lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha familia na jamii zote zinatumia nishati salama kwa afya na kwa ustawi wa vizazi vijavyo.

Dkt. Biteko alibainisha hayo wakati wa Kongamano la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme Machi 4, 2025 jijini Dar es Salaam.

“Nimefahamishwa kuwa Kongamano hili limeanza kwa mjadala mzito juu ya nafasi ya wanawake katika ajenda ya nishati safi ya kupikia ya umeme.

Kupitia mijadala kama hii, tunaibua hoja muhimu na tunashirikiana na wadau wote muhimu kuweka mikakati ya kuhakikisha tunafikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,” Alisema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko aliwataka kutumia fursa hiyo ya Siku ya Mwanamke vyema na kuwasihi wanawake wote kuibeba ajenda hiyo muhimu ambayo, Rais Samia amekuwa akiipa kipaumbele akiwa ndani na nje ya Nchi.

Aliongeza kuwa, kupitia mfuko wa Nishati safi ya kupikia, Serikali itahakikisha kuwa wanawake wanapata mikopo yenye riba nafuu ili waweze kushiriki kikamilifu katika biashara za nishati safi.

Pia, alisema Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa Sera na Sheria mbalimbali zinakuwa rafiki kwa wawekezaji wa nishati safi ya kupikia ili waweze kushiriki kikamilifu katika biashara ya nishati safi​ ya kupikia.

Naye, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewataka Watanzania hususan wanawake kuendelea kuiunga mkono ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watanzania wote.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Gissima Nyamo – Hanga alisema kuwa Serikali imeweka msukumo katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia nishati ya umeme kwa kuwa ni nafuu zaidi na imefika kila mahali nchini.

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO, Balozi Zuhura Bundala alisema kuwa wanawake ndio wahusika wakuu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia. Amesema nishati safi ya kupikia ina gharama nafuu na ni rahisi kwa matumizi.

Jukwaa hilo limelenga kuhakikisha kwamba kila Mtanzania, hususani mwanawake, anapata fursa ya kutumia nishati safi kwa kupikia.