Na Joyce Kasiki,Timesmajira, Dodoma
MAMLAKA ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro imesema katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februari 2025 , watalii wapatao milioni 2.9 wametembelea vivutio vya utalii ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Dkt.Elirehema Doriye, wakati akizungumza na waandishi wa habari jana.
Alisema katika kipindi hicho mapato ya shilingi bilioni 693.959 yamekusanywa na kuingia katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
Kwa Mujibu wa Mkurugenzi huyo ,katika mwaka 2024/2025 ,mwenendo unaonesha Mamlaka itapata watalii zaidi ya milioni moja na mapato zaidi ya lengo ambalo iliweka la kukusanya sh. bilioni 230 huku akisema hadi sasa wameshakusanya asilimia 92 ya lengo.
“Takwimu hizi zinazoonesha kuwa juhudi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia filamu za Royal Tour na Amaizing Tanzania zimechangia kutangaza nchi yetu na kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea vivutio vyetu vya utalii,
“Vile vile mkakati mbalimbali ya Shirika pamoja na ushirikiano kati ya sekta Binafsi na Mamlaka za utalii umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko hili,”alisema .Dkt.Doriye
Aidha alisema katika jitihada za kuboresha huduma za utalii Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro itaendelea kuboresha miundombinu muhimu ikiwa ni pamoja na kuboresha barabara ndani ya Hifadhi ,kuimarisha viwanja vya ndege vya ndani ya Hifadhi,kuboresha kambi za wageni ,kuimarisha Mifumo ya malipo,kuimarisha ulinzi Usalama wa wageni na kuboresha vyoo vya wageni.
Pia alisema katika katika kipindi cha miaka minne kuanzia Januari 2021 Hadi Februari 2025 ,Serikali kupitia Mamlaka hiyo imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara na maji kwa lengo la kuboresha miundombinu ndani ya Hifadhi na maeneo inayosimamia.
***Kuhama kwa hiari ndani ya Hifadhi
Dkt.Doriye alisema kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2022,kumekuwa na ongezeko la watu na mifugo huku akisema wakati Hifadhi hiyo inaanzishwa mwaka 1959 ,idadi ya wakazi ilikuwa takriban 8,000 ambapo wakazi 4,000 tayari walikuwa ndani ya Hifadhi na 4,000 walihamia kutoka Hifadhi ya Serengeti na kwamba mifugo iliyokuwepo ilikadiriwa kufikia 260,000.
“Hata hivyo idadi ya watu na mifugo imeongezeka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni ambapo kwa mujibu wa sensa ya 2022 takwimu zinaonesha kuwa idadi imeongezeka kutoka 261,000 hadi zaidi ya 850,000 huku eneo la hifadhi likibaki na ukubwa ule ule wa kilometa za mraba 8,292 pekee,” alisema Dkt.Doriye
Kutokana na ongezeko hilo la watu na mifugo kumekuwa na changamoto kubwa katika uhifadhi na ustawi wa wakazi wa Ngorongoro huku akisemaili kuboresha maisha ya wananchi na kuwaondoa katika hatari ya kuishi pamoja na wanyamapiri,mwaka 2021 Serikali ilianzisha mradi wa kuwahamisha wananchi kuhama kwa hiari kutoka Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.
Alisema,tangu Juni 2022 lilipoanza zoezi la kuhamasisha wananchi kuhama kwa hiari kwenda Msomera hadi Desemba 2024 maendeleo mbalimbali yamepatikana ikiwemo kaya 1,678 zenye jumla ya watu 10,073 na mifugo 40,593 tayari wameshahama kutoka Ngorongoro kwenda Msomera.
Aidha alisema nyumba 3,003 zimejengwa kwa ajili ya makazi ya wakazi wanaohamia Msomera ambapo nyumba 1,495 zimekwishakaliwa na wananchi waliokwishahama na nyumba 1,508 ziko tayari kwa ajili ya wananchi wengine wakisubiri kukamilika kwa miundombinu ya kijamii.
More Stories
TASHICO yatoa ufafanuzi MV.Victoria kusitisha huduma
Tanzania yang’ara kwa utalii nchi za Ulaya Magharibi
Rais Samia atimiza yote aliyoahidi ALAT 2021