February 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rungwe yajenga soko kukuza uchumi kwa wananchi

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

IMEELEZWA kuwa  katika kuweka  mazingira mazuri kwa wananchi hususani wanawake wanaojishughulisha na ujasiriamali wa mazao, Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya imejenga Soko la kisasa la  Mboga mboga ambalo litawezesha mazingira mazuri  ambayo yatakuza uchumi  pamoja na kuongeza mapato kwa halmashauri

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Februari 22,2025 ,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rungwe na Diwani wa Kata ya Masoko,Mpokigwe Mwankuga amesema kwamba soko hilo litasaidia kuboresha mazingira mazuri ya uuzaji wa mboga mboga kwa wakulima hususani wanawake ambao wamekuwa wakijishughulisha na biashara hizo kwa muda mrefu.

“Halmashauri imeendelea kuweka mazingira rafiki  kwa wananchi wake hasa wanawake kwani  tumeweza  kutengeneza  soko la Mboga mboga  ambapo tumetumia  zaidi ya mil.180 katika ujenzi wa soko hilo ambapo wanawake wanaendelea kuuza mazao yao  hapo hasa mboga mboga  na tumendeelea kuhamasisha wananchi kilimo cha bustani na hata sasa tumepata wafadhili  ambao watakutana na  wizara ya maji  kwa ajili ya kuchimba visima amesema.

Akielezea zaidi Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe  smesema kuwa yapo maeneo machache ambapo kuna wafadhili wamejitokeza kupitia wizara ya Maji wanaenda kuchimba
visima ili watu waweze kujitengenezea bustani za mboga mboga .

Amesema kuwa soko hilo lipo Tandale ambalo halmashauri wakishirikiana na wafadhili ili kuhakikisha wananchi wanaotengeneza mazingira mazuri ya ufanyaji biashara za mboga mboga ambazo zitainua vipato vyao.

Aidha Mwankuga amesema  kwa wilaya ya Rungwe kilimo wanachotegemea zaidi kwa wilaya ya Rungwe ni ndizi hivyo halmashauri imeendelea kuhamasisha kilimo bora na matumizi sahihi ya mbolea ili halmashauri iendelee kupata mapato kupitia ndizi .

Ukipita kila nyumba hutakosa ndizi lakini watalaam wetu bado wanaendelea kuhakikisha matumizi ya mbolea ili na sisi halmashauri tuendelee kupata mapato kupitia kilimo cha ndizi “amesema.

Atuganile Mwamboneke ni mkazi wa Kata ya Kiwira anayejishughulisha na uuzaji wa mboga  katika soko la Tandale amesema kuwa uwepo wa soko hilo umemfanya kubadili maisha yake  tofauti na awali.

“Kupitia biashara yangu hii ya mboga nashukuru Sana maisha yangu yamebadilika na halmashauri yetu ilivyotujengea soko hili imetufanya tupate hamasa zaidi kwani hivi sasa mboga mboga zetu hatupangi chini tena na hata mvua tumeikwepa tupo kwenye jengo zuri kama mnavyojua wilaya yetu hii msimu wote ni wa mvua,” amesema.

Amanyasye Juma amesema uwepo wa soko la mboga mboga itakuwa mkombozi Kwa wananchi wilayani humo hususani wanawake ambao kwa kiasi ndo wamekuwa wakijishughulisha na biashara hizo.