February 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uwindaji wa kitalii kuingizia Tanzania Bil.2.5

UWINDAJI WA KITALII KUIINGIZIA TANZANIA BIL.2.5

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Serikali inatarajia kuingiza jumla ya Dola za Kimarekani 968,000 sawa na shilingi za kitanzania bilioni 2.5 kama ada ya vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa mwaka bila mapato mengine.

Hayo yamesemwa leo Februari 21,2025 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana wakati wa hafla ya kukabidhi vyeti vya umiliki wa Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii kwa wawekezaji watano , iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Ninayo furaha kukabidhi vyeti hivi kwa wawekezaji ambao ni K&F Wild Expedition Ltd (kwa kitalu cha Kilwa Open Area Nakiu), Michel Mantheakis Safaris Ltd kwa (Muhesi GR), Out of Africa Ltd (Lwafi Nkamba), Royal Conservation Ltd (Pololeti GR), na Neon Investment Ltd (Selous MT2) chini ya Uwekezaji Mahiri kwenye Maeneo ya Wanyamapori (Special Wildlife Investment Concession Areas-SWICA)” amesisitiza Chana.

Amefafanua kuwa utoaji wa vyeti hivyo kwa wawekezaji hao wapya unaendana na utekelezaji wa Ilani ya CCM, kutokana na ukweli kwamba hiyo inahalalisha umuhimu wa tasnia ya uwindaji kwa uchumi wa nchi na kusisitiza kuwa Uwindaji wa Kitalii unachangia manufaa ya moja kwa moja kupitia ajira na maendeleo kwa jamii.

Chana ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wengine kutoka China na kwingineko duniani kuwekeza katika Sekta ya Utalii nchini Tanzania huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Mpango wa kuitangaza Tanzania katika kiwango cha kimataifa kupitia filamu za “Amazing Tanzania” na “Tanzania, The Royal Tour”.

“Ninapenda kuwahakikishia wadau wote wa uwindaji wa Kitalii kwamba dhamira ya Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuendelea kuweka na kudumisha mazingira wezeshi ya biashara zao bila kuathiri uhifadhi na ustawi wa watu wetu” amesema Chana.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Meja Jenerali Mstaafu Hamis Semfuko amesema kuwa TAWA imekuwa ikitumia mikakati ya kimasoko kuvutia wawekezaji kutoka duniani kote ikiwa ni pamoja na matumizi ya mnada wa kielektroniki wa kunadi vitalu vya uwindaji wa kitalii ambapo kwa mara ya kwanza imefanikiwa kupata wawekezaji kutoka China katika tasnia ya uwindaji.

“TAWA imejipanga vyema ili kufikia soko la kimataifa na soko la ndani la utalii sambamba na kuangalia uwezekano wa masoko mapya ya utalii kama China, Urusi, India na Brazili” amesema Meja Jenerali Semfuko.

Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mlage Kabange, amefafanua kuwa katika jitihada za kuvutia wawekezaji na watalii zaidi, TAWA itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji.

“Hivi sasa tumejenga kilomita 453.2 za mitandao ya barabara kwa kiwango cha changarawe katika maeneo ya kimkakati sawa na asilimia 40 ya lengo letu ambalo ni kilomita 1,127 ifikapo mwaka 2026, tumejenga miundombinu ya utalii 33 ikijumuisha Banda za watalii, kambi na maeneo ya picnic ambayo ni asilimia 117 ya maeneo yaliyolengwa ya Utalii. Vilevile, TAWA tumefikisha asilimia 23 ya lengo la kujenga vituo 22 vya kukusanyia mapato kama ilivyotarajiwa ifikapo mwaka 2026.

Miundombinu hii ya utalii ililenga kuweka mazingira mazuri na wezeshi ya ufikiaji wa vivutio vyetu vya utalii na kwa lengo la kukuza utalii na kuongeza mapato ya Serikali” amesema Kabange.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allexander Lobora, Mwenyekiti wa Kamati ya Ugawaji Vitalu vya Uwindaji na Mjumbe wa Bodi ya TAWA, Prof. Japhary Kideghesho, Wajumbe wa Bodi ya TAWA, Wawakilishi kutoka Timu ya Majadiliano ya Serikali, Katibu wa Chama cha TAHOA Suleiman Masato na wadau mbalimbali wa Sekta ya Utalii.