February 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia azidi kupewa tano sekta ya uchimbaji madini

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo wa madini kuhakikisha wanapata mitaji, leseni na matumizi ya teknolojia katika shughuli za uchimbaji wa madini na kuwezesha kuchimba kisasa.

Akizungumza katika mahojiano maalum mmiliki wa Mgodi wa Kwasakwasa uliopo kijiji cha Msesule kata ya Mapogoro, wilayani Mbarali mkoani Mbeya, Amagite Mkumbwike, alisema, Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mazingira wezeshi ikiwemo bei nzuri sokoni ili wachimbaji wadogo waweze kunufaika zaidi.

“Nikiwa mchimbaji mdogo na mmiliki wa mgodi wa Kwasakwasa, nitaendelea kumuunga mkono Rais Samia kwa kuendelea kutoa ajira kwa vijana na kurudisha faida kwa kile kinachopatikana katika vijiji vinavyozunguka mgodi wetu,”alisema na kuongeza,

“Serikali imerahisisha vitu vingi ikiwemo kuhakikisha bei ya dhahabu sokoni zinakuwa juu ili wachimbaji wadogo tunufaike. Tumeendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa kurudisha faida kwa jamii ikiwemo kununua vifaa vya shule kwa wanafunzi wa kijiji hiki ambao wameendelea na masomo yao ya elimu ya juu, pamoja na kununua mashine ya umwagiliaji hapa kijijini,”amesema Amagite

Aidha, kwa upande wa Msimamizi wa Mgodi huo Edward Daud ameiomba Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki zaidi kwa wawekezaji ili vijana wengi wapate ajira kutokana na uwekezaji unaofanywa.

“Na sisi vijana tunapoaminiwa sehemu yoyote ile tukapewa kazi basi tuifanye kwa bidii kwa asilimia 100, tuwe waaminifu kwa waliotupa dhamana,”alisema.