Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu 21 kwa tuhuma za kufanya fujo na kutishia uvunjifu wa amani mara baada ya majina ya wagombea Udiwani kutangazwa.
Akizungumza jijini hapa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ACP.Muliro Jumanne,amesama kuwa Agosti 20, mwaka huu, majira ya saa 7 mchana huko eneo la Pasiansi ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilemela Mkoani hapa watu 21 wanadaiwa kuwa sehemu ya mgombea ambaye hakupitishwa na kikao cha kuteua mgombea udiwani kwa tiketi ya CCM Kata ya Nyamanoro.
ACP.Muliro amesema kikundi hicho kilifika eneo la ofisi hiyo kikiwa katika mazingira ya kufanya fujo na kutishia uvunjifu wa amani eneo hilo huku wakiwepo baadhi ya viongozi wa CCM wanaofanya kazi katika eneo hilo.
Amesema mara baada ya Polisi kufika eneo la tukio mtu mmoja anayedaiwa kujilikana kwa jina la Abrahman Khalfan Kange ambaye alishika nafasi ya pili kwenye kura za maoni ya chama hicho alikimbia lakini kundi alilokuwa analihamasisha kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani wa eneo hilo wamekamatwa.
Alisema kuwa wanahojiwa kwa kina na hatua za kisheria zitachukuliwa ili kukomesha tabia na mtindo unaotaka kuzuka wa baadhi ya wagombea wa vyama mbalimbali ambao hawakupata fursa ya kupitishwa kugombea katika vyama vyao kugeuka na kuanza kuhamasisha watu/ vijana kuanzisha vitendo vya vurugu au fujo suala ambalo ni kosa kisheria na haliwezi kupewa nafasi na jeshi hilo.
Hata hivyo alisema jeshi hilo mkoani hapa linaendelea kufuatilia kwa ukaribu shughuli zote zinazohusiana na masuala ya uchaguzi na linawashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaoutoa na kusisitiza kuwa wasifumbie macho vitendo vya uhalifu bali watoe taarifa mapema ili ziweze kufanyiwa kazi haraka na Mwanza iendelee kuwa salama.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea