Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza
Watoto wawili wanafunzi wa shule ya mchepuo wa kiingereza Blessing Model,waliodaiwa kutekwa Februari 5,2025 na watu wasiojulikana wamepatikana huku watuhumiwa wa utekaji huo wakiuwawa kwa kupigwa risasi na Askari wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza.
Akizungumza Februari 8,2025,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa,amesema tukio la utekaji watoto hao lilitokea Februari 5,2025,majira ya saa 12:10 asubuhi eneo la Capripoint katika barabara ya Nassa, Wilaya ya
Nyamagana wakiwa kwenye gari yenye namba za usajili T. 233 DJC Toyota Hiace, mali
ya shule hiyo wakati wanapelekwa shuleni.
Huku waliokuwa wametekwa ni Magreth Thobias Juma(8) mwanafunzi wa darasa la
pili na mkazi wa mtaa wa Hesawa, Capripoint na Fortunata Geofrey Mwakalebela(5) mwanafunzi wa darasa la kwanza na mkazi wa Bugando wote wanafunzi wa shule ya msingi ya mchepuo wa kiingereza ya Blessing Model iliyopo Nyasaka, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Mutafungwa ameeleza kuwa,baada ya tukio hilo jeshi hilo lilianza doria na msako katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza,
kwa kutumia wataalamu wa polisi wa matukio makubwa kwa kushirikiana na wananchi ili
kuweza kuwapata watoto hao wakiwa salama sambamba na kuwakamata waharifu wote
waliohusika na utekaji huo.
Hivyo Februari 08,2025 majira ya saa 6:30 mchana, jeshi hilo lilipata taarifa kuwa
katika mtaa wa Nyabulogoya, Kata ya Nyegezi, Wilaya ya Nyamagana, nyumba namba 8,kuna watu walikuwa wanawashikilia watoto hao bila uhalali huku wakiendelea kutaka
kupewa fedha kutoka katika uongozi wa shule hiyo.
“Kupitia Askari wa kupambana na makosa makubwa ya uhalifu, waliokuwa wakiendelea na msako katika maeneo mbalimbali, mara moja walifika eneo hilo na kuizingira nyumba hiyo kwa lengo la kuwaokoa watoto hao na kuwakamata wahalifu,”ameeleza Mutafungwa na kuongeza:
“Askari wetu waliokuwa na silaha walipojaribu kuingia katika chumba walipokuwa watekaji ambapo walikuwa wanawashikilia watoto, ndipo watu wawili jinsi ya kiume walitoka wakiwa na
panga, jambia na nondo na kutaka kuwashambulia askari.Askari walilazimika
kuwafyatulia risasi zilizowajeruhi watekaji na kuvuja damu nyingi,ambapo walipoteza maisha wakati wa jitihada za kuwapeleka hospitali kwa matibabu,”.
Pia ameeleza kuwa katika tukio hilo watoto waliokuwa wametekwa waliweza kupatikana wakiwa salama na wamechukuliwa na kupeleka hospitali ya Mkoa ya Sekou -Toure na askari wa Dawati la Jinsia na Watoto pamoja na Ustawi wa Jamii,kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa
hali ya afya zao.
Watuhumiwa wawili ambao bado hawajatambulika majina na anwani
zao,walikimbia kutoka eneo la tukio baada ya kuwaona askari,hivyo wanaendelea
kuwatafuta huku miili ya watu wawili ambao wanakadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 hadi 35,imehifadhiwa hospitali ya Sekou -Toure,kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi.
Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza,kuendelea kutoa ushirikiano ili kudhibiti uhalifu na wahalifu,huku akiwatahadharisha watu wanaojiusisha na vitendo vya utekaji na uhalifu mwingine vinavyoleta taharuki kwa wananchi.
“Mkoa wa Mwanza sio sehemu salama kwao, tutawasaka popote pale walipo na kuwachukulia hatua za kisheria,”.
More Stories
Wakuu wa nchi wa EAC,SADC watoa maazimio kumaliza mgogoro wa Congo
Watumishi Madini waaswa kufanya kazi kwa bidii, kuwa wazalendo
Masauni:Biashara ya Kaboni ni Ukombozi kwa Taifa