February 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa:Mfumo wa Anwani za makazi huchochea upatikanaji wa huduma za kijamii

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema mfumo wa anwani za makazi utasaidia kuchochea upatikanaji wa huduma za kijamii, kuimarisha masuala ya ulinzi na usalama, kuwezesha biashara mtandao kufanyika kwa ufanisi na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na majanga.

Hivyo amewataka wananchi kutunza na kuwa walinzi wa miundombini ya anwani za makazi kwani Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika mradi huo.

“Vibao tulivyoviweka kuonesha mitaa na barabara,tunao Watanzania ambao si waaminifu wanang’oa mabango hayo na kwenda kuyauza,ni muhimu kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hiyo kwa sababu ina manufaa”amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema hayo jijini hapa leo  Februari 8,2025 katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi ambapo maadhimisho hayo yamekwenda sambamba na Uzinduzi wa matumizi ya mfumo wa Anwani hizo.

Aidha amesema suala la anwani za makazi ni moja ya masuala yaliyopewa kipaumbele katika Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa Taifa 2021/2022- 2025/2026 ambao umeweka bayana azma ya Serikali ya kujenga mfumo wa anwani za makazi na postikodi katika kata zote nchini.

“Siku kama ya leo tarehe 8 Februari, 2022, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi nchini kwa njia ya operesheni. Operesheni hiyo ilifanyika kwa muda wa miezi minne na kuwezesha ukusanyaji wa taarifa milioni 12.3 za anwani za makazi zilizohifadhiwa katika mfumo wa kidijitali wa anwani za makazi unaojulikana kwa jina la National Physical Addressing (NaPA).

Amesema kupitia programu ya NaPA mwananchi akiwa eneo lolote nchini na hujui sehemu ya kupata huduma za kijamii kama vile kituo cha afya au mgahawa anaweza kutumia programu hiyo kutafuta sehemu za karibu. “Hii ni programu bora na inarahisisha kupata huduma husika sambamba na kwenda na kasi ya kimaendeleo katika uchumi wa sasa wa Kijiditali.”

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Jerry Silaa amesema kuwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea kusimamia na kuendeleza miundombinu na mifumo ya msingi (Foundation Systems), ambayo ni mhimili muhimu wa uchumi wa kidijitali ulioainishwa katika Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa Miaka 10 (2024–2034).

Amesema mifumo hiyo inajumuisha mifumo ya utambuzi wa watu, biashara, ardhi, na makazi. “Katika muktadha huu, utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ni hatua ya kimapinduzi inayolenga kuboresha utambuzi na utoaji wa huduma kwa wananchi hapa nchini.”

Akitoa salamu Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Nadir Abdulatiff Awady amesema zoezi la uwekaji wa anwani za makazi kwa upande wa Zanzibar limekamilika kwa asilimia 100, ambapo kwa sasa wanaendelea kuwahamasisha wananchi kuhusu matumizi ya anwani hizo za makazi.