Na George Mwigulu,Timesmajiraonline,Katavi.
JESHI la Polisi Mkoa wa Katavi linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za wizi wa waya aina ya copper earth road kilovote 33.4 mali ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za upelelezi ni matokeo chanya ya ushirikiano wa TANESCO na Jeshi la Polisi wa kulinda miundombinu mbalimbali ya umeme ambayo ni msingi wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi Kaster Ngonyani,amesema hayo jana February 7, 2025 huku akisisitiza kuwa kupitia doria, misako na operesheni wamefanikiwa kukamata watuhumiwa hao.
Akiwa ofisini kwake, Ngonyani ameeleza kuwa Jeshi hilo haliwezi kufumbia macho wizi wa mali za umma na uhalibifu wa miundombinu hiyo kwani wako imara kwa yeyote atakayehusika na wizi hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Pamoja na kukamata watuhumiwa hao wawili Ngonyani amesema “Kwa kipindi cha mwezi Januari 2025, Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 118 wa makosa mbalimbali, ambapo kati yao watuhumiwa 37 wamekamatwa wakiwa na mali zinazozaniwa kuwa za wizi”
Wizi wa waya umetajwa na maofisa wa TANESCO kuwa ni chanzo cha kukwamisha utoaji wa huduma bora kwa wateja wao huku ukirudisha nyuma juhudi za serikali kuimalisha miundombinu ya umeme na wakati mwingine kusababisha hasara serikali.
Mbali na ukamataji huo, Jeshi la Polisi kwa upande mwingine wamepata mafanikio katika kesi za mahakamani jumla ya watuhumiwa 17 walipatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo mbalimbali gerezani katika kesi zilizokuwa zikiwakabili.
Ngonyani amefafanua watuhumiwa 6 wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kosa la mauaji, mtuhumiwa mmoja amehukumiwa miaka 20 kwa kosa la kupatikana na nyara za serikali, mtuhumiwa mmoja amehukumiwa miaka 7 kwa kosa la kujeruhi, watuhumiwa wawili wamehukumiwa mwaka 1 kwa kosa la kuingia ndani ya hifadhi bila kibali.
Watuhumiwa wengine 7 wamehukumiwa miezi sita kwa kosa la kupatikana na pombe haramu ya moshi na dereva mmoja amehukumiwa kifungo cha nje mwaka mmoja kwa kosa la kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha majeruhi pamoja na uharibifu.
Aidha ametoa rai kwa wananchi kuacha kujihusisha na vitendo viovu vya uhalifu hasa matukio ya kuhujumu miradi ya serikali kwa kuharibu au kuiba pamoja na kujichukulia sheria mikononi huku akiwaomba kutoa ripoti kwa wakati kwa jeshi hilo pindi wanapobaini viashiria vya uharifu.
More Stories
Majaliwa:Mfumo wa Anwani za makazi huchochea upatikanaji wa huduma za kijamii
Serikali:Dawa za ARV haziuzwi,zipo za kutosha
Tanzania kuendeleza mipango ya kidemokrasia kukomesha mzozo na machafuko Congo