February 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbaruku:Lushoto haikutakiwa kuwa na shida ya maji

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Mathew Mbaruku amesema hakutarajia kukauka kwa vyanzo vya maji vya asili katika wilaya hiyo na kuanza kuchimba visima kutafuta maji ardhini.

Amesema kuwa sababu ya kutokea kwa hali hiyo ni uharibifu wa mazingira, huku wananchi wakilima kwenye vilima vyenye vyanzo vya maji na hadi katikati ya mito, na kuongeza kuwa kuna siku hata hayo maji ya visima yatakauka, na itabidi wananchi wapelekewe maji kutoka Tarafa ya Mombo wilayani Korogwe, jambo ambalo halitawezekana.

Mbaruku amesema hayo Februari 6, 2025 wakati anafunga kikao cha Baraza la Bajeti la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, ambapo madiwani walipitisha rasimu ya bajeti ya halmashauri hiyo, rasimu ya bajeti ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), na kuchangia Mpango wa maandalizi ya rasimu ya bajeti ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Lushoto.

Amesema Wilaya ya Lushoto imejaliwa kuwa na misitu ya asili, mito na vijito, huku ikiwa imejaa mabonde yenye ardhi oevu, lakini shughuli na ongezeko la binadamu limefanya baadhi ya vyanzo vya maji kukauka, huku watu wakilima kwenye vilima vyenye vyanzo vya maji, na wengine wakilima kilimo cha mbogamboga hadi katikati ya mito.

Hivyo amewaasa madiwani kuangalia maslahi ya Taifa katika kutunza vyanzo vya maji, na kuwataka wasiwe na wasiwasi katika kuwakemea wananchi wanaoharibu mazingira kwa kuhofia watanyimwa kura, kwani kura zipo tu.

“Sikutegemea siku moja Lushoto tutatafuta maji chini ya ardhi badala ya yale maji yaliyojaa kwenye misitu. Pia, siku moja tunaweza kuletewa maji kutoka Mombo, na sijui hayo maji nao watayatoa wapi! maana kuna uwezekano hata haya maji ya visima yasipatikane

“Madiwani waelezeni wananchi wasilime mpaka katikati ya mito. na msidhani kufanya hivyo ni kujimaliza, bali ni kuweza kulinda vyanzo vyetu vya maji.  Kama kura zipo tu, na wananchi watawachagua,”amesema Mbaruku.

Naye, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga akiwasilisha  Mpango huo wa bajeti, alisema  wamepanga kutekeleza kazi mbalimbali katika mwaka wa fedha 2025-2026, na mategemeo ni kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto itatumia kiasi cha sh. bilioni 5.3 kukamilisha miradi ya maji inayoendelea pamoja na miradi mipya michache.

“Ukamilishaji wa Mradi wa Maji Mnazi, ukamilishaji wa Mradi wa Maji Mkundi Mtae, ukamilishaji wa Mradi wa Maji Lushoto Mjini, ukamilishaji wa Mradi wa Maji Hemtoe-Gologolo, ukamilishaji wa Mradi wa Maji Makole/Kilole/Kwekanga, ununuzi wa bomba na viungo vyake kwa lengo la kutekeleza miradi midogo midogo ya ukarabati, upanuzi wa Mradi wa Maji Bungoi kwenda Kwemshasha.

“Upanuzi wa Mradi wa Maji Mng’aro kwenda Ngwaru, upanuzi wa Mradi wa Maji Ngwelo kwenda Mazashai, ukamilishaji wa Jengo la Ofisi ya RUWASA, kuendelea na zoezi la uchimbaji visima na kufanya usanifu katika maeneo yaliyochimbwa visima, ukamilishaji wa miradi yote ya visima ikiwa ni program maalumu ya kufikisha huduma ya maji vijijini,”amesema Mhandisi Sizinga.

Mhandisi Sizinga amesema pamoja na mapendekezo hayo ya utekelezaji wa miradi, wametoa nafasi ya ushauri na mapendekezo kutoka katika kikao hicho
kwa lengo la kuboresha mapendekezo yao kulingana na mahitaji, na madiwani walichangia na kuelezea changamoto za maji zilizopo kwenye maeneo yao, na namna ya kukabiliana nazo.

Mhandisi Sizinga amesema baada ya Mwangozo kutolewa, utaratibu wa kuandaa Mpango wa Bajeti kwa kuzingatia maoteo ya bajeti kwa mwaka wa fedha uliopita yaani mwaka wa fedha 2024-2025 huanza katika ngazi za Wilaya, ambapo kipaumbele kikubwa ni kukamilisha miradi inayoendelea kutekelezwa.

“Katika mwaka 2024/2025, RUWASA Lushoto ilipangiwa jumla ya sh. 9,181,227,494.  Na kati ya fedha hizo, sh. 20,907,935 ni fedha za matumizi ya kawaida (OC) na sh 9,160,319,559 zikiwa ni fedha za maendeleo. Mpaka sasa Ofisi ya RUWASA Lushoto imepokea jumla ya fedha sh. 1,723,285,777,”amesema Mhandisi Sizinga.