January 30, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampeni ya msaada wa kisheria tumaini la wananchi

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Tabora

Kampeni ya Huduma za Msaada wa Kisheria kwa jamii,imekuwa tumaini na msaada,hivyo wananchi mkoani Tabora wamefurahishwa na kampeni hiyo huku wakimpongeza Rais Samia kwa kuianzisha.

Wakiongea na gazeti hili baadhi ya wazee na wanawake,baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo,uliofanyika uwanja wa Chipukizi Halmashauri ya Manispaa ya Tabora,wamesema hawatumii gharama yoyote na wanaongea ana kwa ana na wataalamu na kutatuliwa malalamiko yao.

Mzee Medeye Chabandi mkazi wa Ipuli Halmashauri hiyo,amesema kampeni hiyo ni nzuri,inasaidia wananchi wasio na uwezo kifedha kupata huduma ya msaada wa kisheria na hatimaye kupata haki zao.

“Mimi nilidhulumiwa kiwanja, nimehangaika kutafuta haki yangu, kila siku nilikuwa napigwa danadana tu na wahusika, lakini leo nimeonana na watoa huduma wa msaada wa kisheria, wamenisaidia na nimeridhika,” amesema.

Cathlyne Moshi mkazi wa Mtaa wa Kanyenye, ameeleza kuwa wamepokea huduma hiyo kwa mikono miwili, kwani wanakumbana na vikwazo vingi wanapokuwa wanafuatilia haki zao na wengine hawana uwezo kiuchumi.

“Wananchi wengi wamekuwa wakipoteza haki zao au kushindwa kuzifuatilia kwa kutokujua taratibu za kisheria au kukosa Mawakili wa kuwatetea kutokana na uwezo mdogo wa kifedha,” amesema.

Akizindua Kampeni hiyo kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Damas Ndumbaro, Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Paul Chacha, amesema kuwa Wizara imejipanga kuhakikisha kampeni hiyo inawafikia wananchi wote hata walioko pembezoni.

Amebainisha kuwa, kampeni hiyo ina umuhimu wa kipekee ,itapanua wigo wa wananchi kupata haki zao za kikatiba na itawajengea uelewa wa masuala mbalimbali ya kisheria ili wasiendelee kuonewa na kudhulumiwa.

“Kupitia kampeni hii,Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amedhamiria kulinda, kukuza na kutetea haki za wananchi wake ikiwemo kukomesha vitendo vyote vya uvunjifu wa haki za binadamu,”ameeleza.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria,Jumanne Sagini, amefafanua kuwa kampeni hiyo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha upatikanaji haki kwa wakati kwa wananchi wote wasio na uwezo wa kugharamia Mawakili.

Amebainisha kuwa Kampeni hiyo ya Huduma za Msaada wa Kisheria ya Mama Samia itatolewa kwa wakazi wa Halmashauri zote 8 za Mkoa huo na takribani kata 40 zitanufaika.