Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
JIJI la Dar es Salaam jana limekuwa kwenye mwonekano tofauti na ilivyozoeleka baada ya kubaki ‘jeupe’ kufuatia Mkutano wa siku mbili Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika ulioanza jana.
Mkutano huo unaohudhuriwa na marais 24 wa Afrika ulianza jana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC).
Tanzania imepata heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Nishati (Africa Energy Summit) utakaofanyika jijini Dar es Salaam jana na leo.
Mkutano huu unaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Katika mkutano huu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndiye mwenyeji wa Marais 24 kutoka nchi za Afrika, wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali 21, na Wakuu wa Taasisi za Kimataifa sita, wakiwemo Rais wa Benki ya Dunia, Rais wa Benki ya Afrika, na Rais wa Taasisi ya Rockefeller.
Aidha, washiriki 2,600 kutoka ndani na nje ya Tanzania wamejisajili kushiriki katika tukio hili kubwa.
Kufuatia mkutano huo mkubwa, wananchi mbalimbali wakiwemo waendeshaji wa vyombo vya usafiri vya bodaboda na bajaj wametii agizo la Serikali la kutoingia katikati ya mji kwa kipindi cha siku mbili za mkutano huo (ambao unaisha leo).
Aidha, watumishi wa umma ambao Serikali imewataka kufanyia kazi zao nyumbani wamefanya hivyo, isipokuwa wale ambao mazingira ya kazi yao yanawahitaji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, ilieleza kuwa wafanyakazi watakaotakiwa kufika maeneo yao ya kazi ni wale ambao mazingira ya kazi zao yanawahitaji kuwa katika vituo vya kazi kama vile watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, sekta ya afya na sekta ya usafiri na usafirishaji.
Licha ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kupiga marufuku bodaboda na bajaji kuingia katikati ya jiji kutokana na mkutano wa kimataifa wa nishati, bajaji wametii agizo, lakini
Hata hivyo baadhi ya bodaboda walionekana wakikatisha maeneo ya katikati ya mji.
Januari 25, 2025, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu lilitangaza kufungwa kwa barabara tisa sambamba na barabara nyingine tisa kwa muda kupisha misafara ya viongozi mbalimbali wanaokuja kutoka nchi mbalimbali kuhudhuria mkutano wa nishati Afrika.
Aidha, Polisi iliagiza bajaji na bodaboda kutoingia katikati ya jiji katika kipindi chote ambacho mkutano huo unafanyika ambacho ni Januari 27 hadi Januari 28, 2025.
Gazeti hili limeshuhudia maeneo mbalimbali ilishuhudia bajaji zinazotoka maeneo ya Kimara na Mbezi zikiishia Jangwani, lakini bodaboda zilionekana zikikatiza mitaa kadhaa ya Posta na Kariakoo, ingawa
Bodaboda zilionekana zimebeba abiria waliokuwa wakiwashusha katika mitaa mbalimbali, ikiwemo ya Posta, ambapo baadhi ya barabara zilifungwa ili kupisha misafara ya marais wa mataifa ya Afrika wanaohudhuria mkutano.
Kikubwa ambacho kimeelezwa na abiria ambacho kiliwafanya hadi bodaboda kukaidi agizo a Polisi ni nauli, ambayo ilipanda hadi kufika sh. 17,000 kutoka Ubungo hadi Posta.
Wakati baadhi ya waendesha bodaboda walilalamikia hali ya biashara kutokana na zuio hilo, hali ilikuwa tofauti kwa waliokaidi agizo la Polisi ambapo walisikika wakisema jana ilikuwa siku ya kupga hela.
Hata hivyo, walikiri kuwa hali ya biashara sio nzuri hadi mkutano huo utakapomalizika leo. Wakati hayo yakiendelea maeneo mengi ikiwemo eneo la mkutano walitanda askari polisi waliokuwa wakifanya doria maeneo mbalimbali.
Katika viunga vya Posta Polisi wengine walikuwa kwenye magari kwa ajili ya kuimarisha ulinzi, japo hali ilikuwa shwari.
Mabasi ya mwendokasi yalikuwa yakiendelea kutoa huduma ya usafiri kama kawaida, hasa kwa kwenda maeneo ya jiji kwa kuzingatia kwamba yana njia zake.
Teksi zinazoitwa na watenja kwa njia ya mtandao hazipatikani kirahisi kutokana na kuwa na idadi kubwa ya abiria.
Wananchi wengi walisema abiria walikuwa wengi kuliko teksi, huku bajaj na pikipiki zikiwa zimepigwa kuingia mijini.
Baadhi ya bodaboda waliozungumza na gazeti hili walisema, Daud Michael, alisema hawaenda mjini katika siku hizi mbili za mkutano, kwani hawezi kupingana na kauli ya polisi.
Wakati hayo yakiendelea Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeongeza treni mbili za safari katikati ya jiji hilo ili kukidhi mahitaji ya usafiri.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano, Fredy Mwanjala, imezitaja treni hizo kuwa ni za Stesheni ya Kamata na Pugu.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa treni hizo zitafanya safari zake saa 12:00 asubuhi kutoka Kamata na saa 12:05 jioni kwenda Pugu.
“Shirika la Reli Tanzania linapenda kuwatangazia kuwa, kutokana na kufungwa kwa barabara za kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam kufuatia mkutano wa nishati wa wakuu wa nchi za Afrika, shirika limeongeza treni mbili za mjini kati ya Stesheni ya Kamata na Pugu jijini Dar es Salaam kwa tarehe 27 na 28, Januari 2025,” imeeleza taarifa hiyo.
Mwanjala amesema kuwa, pamoja na hatua hiyo, ratiba za awali za treni zitabaki kama kawaida.
Ameongeza kuwa treni hizo za ziada zitafanya kazi kwa saa zilizotajwa pekee, kipindi ambacho abiria wengi huenda kazini asubuhi na kurejea nyumbani jioni.
More Stories
THBUB yatoa tamko kulaani mauaji ya Jumanne Juma
Dkt. Biteko aongoza waombolezaji kuaga miili ya wanafunzi waliofariki Geita
Bungua mweusi anayeshambulia zao la kahawa aibuka Bukoba