January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMA kuendelea kufuatilia mifumo yake

Na Bakari Lulela,Timesmajiraonline,Dar 

MAMLAKA ya hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya Hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika ili kutoa taarifa sahihi kwa wakati kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu athari zinazoweza kujitokeza.

Akizungumza jijini Dar es salaam mbele ya waandishi wa habari Kaimu Mkurugenzi Mkuu Dkt.Ladislaus Chang’a amesema mwenendo wa mvua za msimu (Novemba 2024 Hadi Aprili, 2025) ambazo utabiri wake ulitolewa mwezi Oktoba, 2024 zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini katika maeneo ya Kigoma, Katavi, Rukwa, Songwe , Singida na Dodoma Kaskazini na mashariki mwao mikoa ya Mbeya na Iringa.

“Mvua hizi zilianza mapema wiki ya nne ya Oktoba na wiki ya kwanza ya Novemba 2024 katika maeneo mengi ya magharibi mwa nchi kama ilivyotabiriwa. Hata hivyo, mvua zilianza kwa kuchelewa katika maeneo machache ya ukanda wa kusini katika wiki ya kwanza ya mwezi Disemba,2024 katika maeneo mengi,” amesema Chang’a.

Aliendelea kueleza kuwa katika kipindi cha msimu wa  Februari hadi Aprili 2025 mvua zinatarajiwa kama ilivyotabiriwa mwezi Oktoba 2024 msimu wa mvua za za masika ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro) Pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mkoa wa Pwani (ikijumuisha visiwa vya  mafia.

Aidha mikoa ya Dar es salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba ukanda wa ziwa Victoria (mikoa ya Kagera,Geita , Mwanza , Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma

TMA imeeleza kuwa kutokana na mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa katika kipindi cha Masika mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na mashariki mwa mikoa ya Mara na Simiyu

Aidha mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya Pwani ya kaskazini, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na ukanda wa ziwa Victoria (mikoa ya Kagera , Geita Mwanza Shinyanga na Magharibi mwa mikoa ya Simiyu na Mara) katika kipindi cha msimu wa masika 2025. Ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi April 2025.