Na Penina Malundo,Timesmajira
MAMLAKA ya Vitambulisho va Taifa(NIDA),imesema kuwa imeendelea kuwatumia ujumbe mfupi wa simu (sms)wahusika wa vitambulisho ambavyo havijachukuliwa kwenda kuchukua vitambulisho vyao kwa muda ulioelekezwa endapo wasipofika kwa muda huo matumizi ya namba zao za utambulisho wa taifa (NIN)yatasitishwa.
Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa NIDA, James Wilbert wakati akizungumza na waandishi wa habari alisema kumekuwa na kusuasua kwa wananchi kwenda kuchukua Vitambulisho vyao ingawaje tayari washapata ujumbe mfupi kwa njia ya simu.
Amesema kusitisha matumizi ya Namba za Utambulisho unalenga kwa wahusika wale ambao watakuwa wamepata ujumbe huo mfupi wa simu halafu wakaacha kujitokeza kwenda kuchukua vitambulisho vyao.” Wewe kama hukupata sms kukujulisha kuwa kitambulisho chako kipo ofisi ya NIDA ya wilaya fulani Namba yako haitazuiwa.
”Dhamira ya serikali ni kuona kila kitambulisho kilichotengenezwa kinachukuliwa na mhusika na hasa ikizingatiwa vimeigharimu serikali pesa nyingi kuvitengeneza,”amesema na kuongeza
”Ujumbe huu utaendelea kutumwa kwa wananchi wote ambao hawakua wamechukua vitambulisho vyao hivyo wananchi waendelee kuwa wavumilivu kwani kila mwananchi ambaye hajachukua kitambulisho na amesajili namba ya simu atatumiwa SMS,”amesema.
Wilbert alisema mara baada ya kufanya utafiti kutaka kujua kwa nini wahusika hawajitokezi kuchukua Vitambulisho vyao hivyo walibaini mambo mbalimbali ikiwemo baadhi ya wananchi kwa makusudi kutojali kuchukua vitambulisho vyao kwa kuwa wana Namba za Utambulisho yaani NINs hivyo kupata huduma zote sawa na mwenye Kitambulisho pale anapohitaji huduma zenye sharti la kuwa na Kitambulisho cha Taifa au Namba.
”Pia tumebaini baadhi ya wananchi wamehama kutoka sehemu waliyokuwa wanaishi wakati wanajisajili na ambako ndiko vitambulisho vyao vimepelekwa na kwenda sehemu nyingine, hii ni pamoja na wanafunzi waliokuwa shuleni au vyuoni kumaliza masomo yao na kwenda sehemu nyingine huku baadhi ya wananchi wengine tayari wamefariki,”amesema.
Amesema kwa kuwa ni wajibu na jukumu la NIDA kuhakikisha kuwa Vitambulisho vyote wanavyochapisha vinachukuliwa na wahusika, na kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Innocent Bashungwa alipotembelea NIDA Disemba 17,2024 ya kuhakikisha kuwa ndani ya miezi miwili vitambulisho vyote 1,200,000 vilivyokuwa katika ofisi za Kata, Vijiji, Mitaa, Vitongoji na Shehia viwe vimegawiwa na kuchukuliwa na wahusika.
Aidha Wilbert alisema baada ya maagizo hayo NIDA iliweza kukusanya vitambulisho vyote vilivyokuwa katika ofisi hizo nchini kote na kuvirudisha katika ofisi zao za wilaya,ingawaje hapo mwanzo vilikua vinachukuliwa Kata, Vijiji, Serikali za Mitaa na Vitongoji ambapo muitikio ulikuwa mdogo uliosababisha zaidi ya vitambulisho 1,000,000 kuendelea kubaki katika ofisi hizo kwa muda mrefu.
Uamuzi wa kuvipeleka Vitambulisho wilayani umekuja mara baada ya wananchi kulalamika juu ya changamoto wanazokutana nazo kutoka ofisi hizo na wengine kushindwa kupata Vitambulisho vyao na kurudi kudai wilayani.
Amesema wapo baadhi ya wananchi ambao wakati wanajisajili vitambulisho hivyo walikuwa mahali au eneo tofauti na wanapoishi sasa ambako ndiko walisema watachukua vitambulisho vyao na ndugu na jamaa kwa utaratibu.
”Sharti pekee tuliloliweka ni huyo mtu anayekwenda kumchukulia Kitambulisho chake aende akiwa na meseji tuliyoituma kwa huyo mwenye Kitambulisho na namba ya NIDA kwa anayechukuliwa na anayemchukuliwa mwenzake.
Hivyo, kusiwe na kisingizo chochote kuhusu mtu kutokuwepo katika eneo lake la awali ambako ndiko Kitambulisho chake kilikuwa kimepelekwa, anaweza sasa akamtuma mtu kwenda kumchukulia katika ofisi ya Wilaya ya NIDA alikokuwa wakati anajisajili,”alisisitiza.
Akizungumzia Vitambulisho vilivyofutika amesema tayari NIDA iliwatangazia wananchi wote wenye vitambulisho vyenye changamoto hiyo kuvirudisha katika ofisi za NIDA za Wilaya au katika ofisi za Kata, Vijiji, na Mitaa vilikokuwa vimepelekwa.
Amesema NIDA inaendelea na zoezi hilo la kukusanya Vitambulisho vyote vyenye changamoto kwa ajili ya kuvichapisha tena.
”Naomba nitoe wito kwa kwa mwananchi yeyote ambaye Kitambulisho chake kitakuwa na changamoto ya kufutika tafadhali akirejeshe katika ofisi ya NIDA ya Wilaya anayoishi lengo la kuvichapisha upya na kugawiwa kwa wahusika bure bila malipo yeyote,”amesema.
More Stories
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais
Dkt.Kafumu:Uteuzi wa Rais Samia umezingatia katiba