January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Kafumu:Uteuzi wa Rais Samia umezingatia katiba

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline,

KAMISHNA wa zamani wa madini na mbunge wa zamani Jimbo la Igunga Dkt.Peter Kafumu, amesema kuteuliwa kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu ujao ni sahihi  na umezingatia matakwa ya katiba ya chama chao.

Hivi karibuni wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa uliofanyika Jijini Dodoma walimpitisha Rais huyo kwa mara ya kwanza kushiriki mchakato wa kugombea urais kwa kwenda kupigiwa kura ili kuwania nafasi hiyo kwa muhula mwingine.

Dkt.Kafumu Januari 20, 2025 ameweka wazi kuwa umahili, uwajibikaji na uzalendo kwenye usimamizi wa rasilimali za nchi kwa maendeleo ya watu alionao amesitahili kuwa mgombea wa nafasi hiyo ya juu zaidi ya mamlaka  licha ya utaratibu wao  unaruhusu kugombea awamu nyingine ya pili na kuongoza kwa miaka mitano.

Mtaalamu huyo wa Jiolojia akiwa jijini Dar es salaam amezungumza kuwa katika usimamizi wa rasilimali za madini  kwa kipindi cha miaka minne akiwa kama mdau kwenye sekta hiyo ameona mabadiliko makubwa yakifanywa hususani ya utekelezaji wa sera ya kufanya madini yanaingia kwenye uchumi wa wananchi kwa maana ya kuongeza thamani yake hapa hapa nchini.

“Kwa mfano katika mgodi wa Kahama wa Bulyakuru wanataka kujenga mtambo wa kusafisha madini ya kopa ili tusafishe kopa wenyewe na kuuza nje pamoja na madini ya mikeli yanayotoka Kabanga na miradi mingine ya madini yatachakatwa hapa hapa” amesema.

Amefafanua sera hiyo ya madini inaingia kwenye dira ya maendeleo ambapo kutakuwa na mambo makubwa ambayo madini yasaidie kuendeleza viwanda vya Tanzania kwa kuyachakata hapa hapa.

Akizungumzia falsafa za 4Rs za Rais Dkt Samia kwenye ukuaji wa sekta ya madini nchini amesema amefanya mapatano ya raia kwenye Nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii ambapo mapatano hayo yamewaleta pamoja makundi yote kufanya kazi ya wachimbaji wakubwa na wadogo wa madini kwa kushirikiana kuliko hapo awali.

“Hapo zamani mchimbaji mdogo alikuwa anamchukia sana mchimbaji mkubwa kwamba wanavamia maeneo yao..lakini falsafa hii ya Rais Dkt.Samia imetufanya kuona umuhimu wa kuhitajiana kwa makudi yote kujenga uchumi wa nchi yetu,”amesisitiza.

Ameongeza “ameimarisha hali ya wawekezaji kujiamini pamoja na kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa maana ya kuwapa masoko kila mkoa na wachimbani wadogo kuweza kupata fursa ya kuuza madini”

Jambo linalofanyiwa kazi kwa sasa ni wachimbaji wadogo kupata mitaji ambapo Rais Dkt Samia analisimamia vizuri kwa sababu zile sheria zilizotungwa mwaka 2017  zinawashirikisha wananchi  jambo ambalo ni zuri limefanywa ili kujenga uwiano kwa wawekezaji na wananchi kudhibiti migogoro.

Dkt.Kafumu,amesema wanaimani na Dkt.Samia kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ambapo ni pamoja na kuimarisha sekta ya elimu, afya,maji,umeme,nishati, uchukuzi,kilimo na uvuvi ambayo yanajenga imani.

Pamoja na kuimarika kwa sekta hizo ameweza kutekeleza kwa vitendo miradi ambayo imeachwa na mtangulizi wake imekamilika kama vile SGR, Daraja la Busisi na bwawa la mwalimu Nyerere yote yanaakisi uwezo na umahili wake ambapo kwa miaka mingine mitano makubwa zaidi atafanya.

Katika hatua nyingine amepongeza kuchaguliwa kwa Katibu Mkuu wa CCM,Dkt. Emmaniel Nchimbi kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu utakao fanyika Oktoba 2025 ndani ya chama hicho na kuteuliwa kwa Stephen Wasira kuwa Makamo wa Mwenyekiti CCM bara utakuwa chachu ya ushindi kutokana na uzoefu mkubwa wa kisiasa na uongozi wa ndani na nje ya nchi walionao.