January 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

15 mbaroni tuhuma wizi wa shehena ya unga wa sembe

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

WATU 15 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na  mali ya wizi ya Shehena ya Unga wa Sembe uliokuwa ukisafirishwa kuelekea nchini Malawi baada ya Gari lililokuwa likisafirisha unga huo kuacha njia na kusababisha majeraha kwa dereva wa Lori hilo .

Akitoa taarifa  kwa waandishi wa habari  Januari 17,2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema kuwa tukio hilo limetokea January 15, 2025 majira ya saa 2.00 asubuhi katika eneo la Mlima Kanyegele lililopo Kata ya Kiwira, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe katika Barabara kuu ya Mbeya kuelekea Tukuyu.

Kamanda Kuzaga amesema kuwa lori yenye namba za usajili LA10214 aina ya Freight Liner lililokuwa likiendeshwa na Dereva aitwaye Damson Vincent(35) mkazi wa Lilongwe Malawi ambalo lilikuwa likitokea  Mbeya kuelekea Malawi likiwa limebeba shehena ya Unga wa Sembe liliacha njia na kusababisha majeraha kwa Dereva wa Gari hilo.

Aidha Kamanda kuzaga amesema  kati ya wanaoshikiliwa na polisi, Mussa  Mwile (28) mkazi wa Kanyegele Wilaya ya Rungwe na wenzake 14.

Hata hivyo Kuzaga amesema baada ya ajali hiyo, wananchi wa Kijiji cha Kanyegele na Vijiji jirani vya Mpandapanda na Igula walifika eneo la ajali na kuanza kuiba Unga wa Sembe uliokuwa kwenye mifuko ya kilogramu 25 ipatayo 1253 na kutoweka nayo Kwa kutumia usafiri wa Pikipiki maarufu bodaboda.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Mussa  Mwile na wenzake 14 wakiwa na vielelezo Unga wa Sembe ulioibwa mifuko 65 mizima na minne ikiwa nusu, turubai mbili za gari hiyo pamoja na Pikipiki saba zilizokuwa zikitumika kubeba na kusafirisha mali hiyo ya wizi.

Pikipiki zilizokamatwa ni MC 887 CVY Kinglion, MC 511 DCW Kinglion, MC 137 EMW Kinglion, MC 326 EDK Kinglion, MC 800 BBW T-better na Pikipiki mbili ambazo hazina namba za usajili.

Akielezea  chanzo  cha tukio  ni kujipatia kipato kwa njia isiyo halali. msako unaendelea ili kuwapata watuhumiwa wengine na vielelezo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa baadhi ya wananchi wenye tabia ya kukimbilia eneo la ajali pindi magari yanapopata ajali na kuanza kuiba mali kuacha mara moja kwani ni kinyume cha sheria  na  ni hatari kwa usalama wao.

Kuzaga ametoa  wito kwa wananchi wenye taarifa za mtu au watu waliohusika kuiba na kuficha mali hiyo kutoa taarifa ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.