Joyce Kasiki na Agnes Alcardo,Timesmajira online,Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (CCM) Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa onyo kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za Uongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao kuacha kufanya kampeni kabla ya muda wa kufanya hivyo kufika .
Mwaka huu mwishoni Taifa litaingia katika Uchaguzi Mkuu wa Rais,Wabunge na madiwani ambao wawakilishi wa wananchi.
Aidha amekemea makundi ndani ya Chama hicho huku akisema hayana Afya kwa mustakabali wa chama chao.
Akifungua Mkutano Mkuu wa CCM Taifa unaoendelea jijini Dodoma katika ukumbi Jakaya Kikwete Dkt.Samia amesema Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakienda majimboni na kufanya kampeni jambo ambalo amesema ni kinyume na taratibu walizojiwekea.
“Wanataka kugombea tunakemea kampeni za mapema, tayari tumeshapata malalamiko na ushahidi wa picha za watu wanafanya safari majimboni,wanafanya Mikutano na vitu mbalimbali vinavyoashiria kampeni.”amesema Dkt.Samia
Pia amewataka viongozi na watendaji wa CCM kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi ya kuwatumikia wananchi katika kutatua kero zao.
“Nawataka viongozi na watendaji ndani ya Chama muache kufanya kazi kwa mazoea ,hiki ni chama kikubwa kinachotegemewa .”
Aidha amewataka viongozi wakasikilize wananchi na kutatua shida zao huku akisema kazi hiyo bado haijafanywa kwa uadilifu.
Dkt.Samia pia amekemea makundi ndani ya Chama huku akisema hayana afya katika kukijenga CCM.
“Tunasema makundi ndani ya chama wakati wa kuomba nafasi ni kawaida,lakini tunapopata wagombea wa chama chetu makundi hayo yasiendelee ,na niseme tu sasa tutaanza kuteua wagombea wanaokubalika na kutounda makundi ndani ya Chama”amesema
katika hatua nyingine amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha ama kurekebisha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura wakati ukifika.
Awali Katibu Mkuu wa CCM Taifa Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi amemahukuru Rais Dkt.Samia kwa kumwamini na kumpa nafasi hiyo.
“Nina mwaka mmoja tangu niteuliwe kushika nafasi hii na huu ni Mkutano wangu wa kwanza nikiwa kwenye nafasi hii,hivyo natonashukrani zangu za dhati kwa wadhifa huu.”
More Stories
‘Ni Wasira ‘Makamu Mwenyekiti CCM Bara
15 mbaroni tuhuma wizi wa shehena ya unga wa sembe
Hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wanaohatarisha usalama Mbeya