January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwabukusi akemea wanasiasa wanaotoa kauli za kibaguzi kuelekea uchaguzi mkuu

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira, Dar es Salaam

RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amekemea tabia za wanasiasa na viongozi wanotumia lugha za kebehi, udini, jinsia na ukabila, kubeza wagombea kwasababu zinaligawa Taifa na badala yake wajenge hoja zenye mashiko. 

Aidha, alitolea mfano wa kauli alizotolewa dhodi ya Rais Samia Sukuhu Hassan na mmoja wa wanasiasa wa upinzani na kudai zina lengo la kuligawa Taifa na si kujenga umoja na mshikamano.

Mwambukusi ameyasema hayo leo Januari 13, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala yanayoihusu nchi katika kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Amesema “Kuelekea kipindi cha uchaguzi ni muhimu kuelewa kwamba sheria na katiba yetu ni nyenzo za kulinda demokrasia. “Tumeshuhudia changamoto zinazohusiana na kauli na vitendo vyenye mwelekeo wa kibaguzi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa, hii inapaswa kukomeshwa mara moja.”

Amesema amepokea malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali na ushahidi wa kauli mabazo hazitamkiki zenye nia ovu ya kuwagawa Watanzania. 

Amewataka viongozi wote wa kisiasa kuzingatia misingi ya sheria, kuepuka kugawanya wananchi na kujenga mazingira ya umoja wa utaifa. 

Aidha, amewataka viongozi wastaafu, wa dini na mila kukemea kauli hizo bila kujali itikadi zao kwasababu hazijengi umoja na mshikamano wa Taifa.