Na Penina Malundo,Timesmajira
SERIKALI imeitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA) kuhakikisha kuwa inazingatia masharti ya kulipia mirabaha inayohusiana na matumizi ya muziki katika maeneo ya viwanja vya ndege.
Huku ikitakiwa kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya nyimbo zinazopigwa ni za Tanzania na asilimia 20 ndio za nje ya Tanzania.
Hatua hiyo imekuja leo baada ya ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA)kusaini makubaliano ya ushirikiano (MOU) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA) ya kulipia mirabaha kutokana na Matumizi ya kazi za Muziki wa wasanii wa Kitanzania
Akizungumza leo jijini DaresSalaam katika hafla hiyo ,Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma amesema makubaliano hayo yaliyoingiwa baina ya Taasisi hizo mbili yatasaidia kuhakikisha kuwa wasanii wa muziki wanapata haki yao ya malipo kutokana na matumizi ya muziki katika maeneo ya viwanja vya ndege nchini.
Amesema ni hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa wasanii wanapata masoko ya kazi zao na kupata mapato kutokana na vyanzo mbalimbali vya kazi zao, na kwamba haki zao zinaheshimiwa kikamilifu.
“Hatua hii ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo katika kuhimiza maendeleo ya sekta ya sanaa na muziki nchini,”amesema.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Uchukuzi,David Kihenzile amesema ni hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa wasanii wanapata masoko ya kazi zao na kupata mapato kutokana na vyanzo mbalimbali vya kazi zao.
Kihenzile amesema wajibu uliobaki kwao ni kuona kuwa wasanii wanaendelea kuzalisha kazi zao kwa wingi na kwa ubora unaotakiwa huku wakizingatia aina na ukubwa wa doko au platform watakayopata kupitia viwanja vya Ndege nchini.
“Natoa pongezi kwa Cosota na Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kubuni na kusimamia ipasavyo utekelezaji wa agizo hilo la Rais Samia hivyo natoa wito kwa taasisi zetu zote za Wizara ya Uchukuzi ikiwemo ikiwemo TRC,TPA ,LATRA na TASHICO kuwasiliana na COSOTA na kuiga mfano mzuri iliowekwa na TAA.
Makubaliano hayo yalisainiwa na Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki COSOTA,Doreeb Sinare na Mkurugenzi Mkuu wa TAA,Abdul Mombokaleo wakishuhudiwa na Manaibu waziri wa Wizara hizo mbili ambazo zipo chini yao.
More Stories
Tanzania Mwenyeji wa Mkutano wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika
Watatu mbaroni kwa tuhuma za mauaji wakigombania shamba
Ng’ombe 10 wamekufa kwa kupigwa na radi