Na Allan Kitwe,Timesmajiraonline,Tabora
WATUMISHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Mkoani hapa wametakiwa kutimiza majukumu yao ipasavyo ikiwemo kuhakikisha mapato yote yanayokusanywa kutoka vyanzo mbalimbali yanafikishwa benki.
Onyo hilo limetolewa Januari 9,2025 na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ambaye ni diwani wa Kata ya Ilege, Tarafa ya Ulyankulu, Raphael Lufungija alipokuwa akiongea na Mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake.
Amesema kuwa halmashauri hiyo ni miongoni mwa halmashauri zilizopata mafanikio makubwa sana kutokana na utendaji mzuri wa wataalamu wake na timu nzima ya mapato lakini hataki utendaji wa mazoea.
Amesisitiza kuwa kama kila mmoja atasimama kwenye zamu yake na kufanya kile kinachotakiwa halmashauri hiyo itaendelea kupiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo ikiwemo kufikisha zaidi ya sh bil 10 ya mapato kwa mwaka.
“Katika hili la mapato bado kuna dosari, baadhi ya watendaji wamekuwa wakikusanya fedha na kukaa nazo mifukoni, hili halikubaliki, yeyote atakayebainika kufanya upuuzi huu achukuliwe hatua”, amesema.
Lufungija amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Jerry Mwaga kulisimamia ipasavyo ikiwemo kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinatolewa taarifa na kufikishwa benki mara moja na sio kukaa mifukoni mwa watu.
Amefafanua kuwa fedha za mapato ya ndani ni kichocheo kikubwa kwa maendeleo ya wananchi, hivyo akaitaka timu ya ukusanyaji mapato na wataalmu wote kuacha kufanya kazi kwa mazoea, vinginevyo watakiona cha moto.
“Halmashauri yetu iko vizuri, tuna uwezo wa kukusanya zaidi ya sh bil 10 kwa mwaka kama kila mmoja atatimiza wajibu wake ipasavyo, kikubwa tubadilike na tuache kufanya kazi kwa mazoea,”ameonya.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Jerry Mwaga ameahidi kufanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti na kubainisha kuwa tayari wameshaanza kuchukua dhidi ya wote wanaokwamisha mapato ya halmashauri.
Mwaga amesisitiza kuwa watendaji na timu nzima ya mapato wanapaswa kushirikiana ipasavyo ili kuhakikisha mapato ya halmashauri hiyo yanaendelea kuongezeka zaidi ili kuvuka lengo lao la kila mwaka.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi