Na Allan Kitwe,Timesmajiraonline,Tabora
SERIKALI imeelekeza shule zote nchini kuhakikisha zinaunda Kamati za Ulinzi wa Watoto ili kukabiliana na vitendo vya ukatili na maadili yasiyofaa kwa watoto ambayo hupelekea kuiga tabia mbaya hivyo kushindwa kutimiza ndoto zao.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt Doroth Gwajima Januari 9,2025 alipokuwa akiongea na wakazi wa Jimbo la Ulyankulu, Wilayani Kaliua katika siku ya moja ya ziara yake Mkoani hapa.
Amesema kuwa serikali ilishatoa Mwongozo wa kuundwa Kamati za Ulinzi wa Watoto katika shule zote hivyo ni muhimu sana Kamati hizo zikaanzishwa shule zinapofunguliwa ili watoto wanasome na kumaliza wakiwa na maadili mazuri.
Waziri Gwajima amesisitiza kuwa Kamati hizi zitasaidia sana kumlinda mtoto na vitendo vya ukatili ikiwemo kumwepusha kujiingiza katika michezo michafu ya ulawiti, usagaji, ushoga na mingineyo.
Aidha amewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kukaa na watoto wao vizuri, kuwafundisha maadili mema na kutowafanyia vitendo vya ukatili wa kijinsia ili wasome vizuri na wakue katika maadili mema na hatimaye watimize ndoto zao.
‘Mtoto anapofanyiwa vitendo vya ukatili, kulawitiwa,kubakwa au kufundishwa mambo yasiyo ya kimaadili ataharibika mapema sana na hataweza kutimiza ndoto za maisha yake, naomba sana tuzingatie hili ili kujenga jamii iliyo bora’, ameeleza.
Dkt Gwajima amepongeza kazi nzuri inayoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuboresha miundombinu ya shule zote nchini hivyo akaomba watoto watumie vizuri miundombinu hiyo.
‘Watoto wakijifunza tabia mbaya hata haya madarasa mazuri, matundu ya vyoo, maabara na mabweni yanayojengwa na serikali watayatumia vibaya, nawaombeni sana tuwalinde na vitendo vyovyote visivyo vya kimaadili’, ameshauri.
Mbunge wa Jimbo hilo Rehema Migira amemshukuru Rais Samia kwa kuwaletea zaidi ya sh mil 361 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi Langoni na sh mil 136 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya sekondari Mkindo.
Shule ya Langoni itasaidia sana kupunguza msongamano wa watoto katika shule mama ya Ibambo na kero ya kutembea umbali mrefu watoto wa kike wanaotoka katika Kitongoji cha Songambele, Kijiji cha Ibambo Kata ya Mwongozo.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi