January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Rungwe

WANANCHI wa Kata ya Kisondela wilayani Rungwe mkoani Mbeya wameishukuru serikali kwa ujenzi wa Shule mpya ya Ufundi ya Amali iliyopo kwenye kata hiyo na kusema  kuwa imeongeza ajira pamoja na kuchavusha uchumi  kwa  watumishi  na wanafunzi wa shule hiyo katika  kunufaika na bidhaa za kilimo zinazopatikana kwenye eneo hilo .

Wamesema hayo leo Januari 9,2024 wakati Mkuu wa wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya,Jaffar Haniu alipofanya ziara na kukagua na hatua za ujenzi wa shule ya Amali ya Ufundi iliyopo kwenye kata hiyo.

Amanyisye Kalinga  ni mkazi wa Mpugha kata ya kisondela amesema kuwa kufuatia uwepo wa ujenzi huo kumekuwa mabadiliko makubwa ya kiuchumi katika eneo hilo ambalo wakazi wake wanajishughulisha na kilimo.

Haniu pamoja na mambo mengine ameridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa na kuwa hii itasaidia ukuaji wa maarifa na ujuzi kwa wakazi wa wilaya ya Rungwe  pindi ujenzi utakapokamilika.

Aidha Haniu ameagiza mafundi wanaotekeleza mradi huo kufanya kazi usiku na mchana ili kusaidia ukamilishaji  wa  ujenzi wa shule hiyo kwa wakati.

“Ndugu zangu hakikisheni ujenzi huu unakamilika kwa wakati ili Shule hii iweze kuanza mapema na watoto wetu waweze kuanza masomo yao mapema”amesema Mkuu huyo wa Wilaya.

Jumla ya Shilingi Million 583 zimetolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ambapo Baraza la Madiwani tayari limetoa azimio la kusajiliwa kwa jina la Renatus  Mchau mara  baada ya ujenzi wake utakapokamilika.

Kata ya Kisondela ni maarufu kwa kilimo cha ndizi, parachichi,machungwa, mahindi na karanga ambapo kimekuwa kilimo maarufu kwa kuwaingizia kipato wananchi.