Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Serikali ya Tanzania imeihakikishia Serikali ya Uingereza kuendeleza ushirikiano kwenye sekta ya madini hususani katika kujengea uwezo watu wake, kubadilishana uzoefu, uongezaji thamani madini na kuwekeza kwenye kufanya tafiti mbalimbali ili kukuza sekta ya madini na kupanua mnyororo wa thamani ili kuongeza ajira na kuchangia katika ukuaji wa pato la taifa.
Hayo, yameelezwa Jana na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde katika ofisi ndogo za Wizara ya Madini jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania,Marianne Young.
Amesema Tanzania na Uingereza zimekubaliana katika kuwajengea uwezo watu wake na kubadilishana uzoefu hususani katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini nchini (GST) na British Geological Survey (BGS)ya Uingereza ili kuwajengwa uwezo Watanzania kwakuwa na ujuzi stahiki katika masuala ya uendelezaji wa sekta ya madini
Amesema eneo la pili walilozungumza kwa urefu ni katika madini mkakati ambapo Uingereza wameonesha utayari katika kushirikiana na Tanzania katika eneo la mnyororo mzima wa uongezaji thamani madini mkakati ambapo Tanzania imejipanga kuhakikisha inavutiwa uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani madini hapa nchini.
Sasa ni muda muafaka wa kuhakikisha “madini ya kimkakati yanawanufaisha Watanzania na taifa, na ndiyo maana tumeandaa Mkakati maalumu wa kutekeleza azma hiyo huku ikizingatiwa kuwa madini hayo kwa sasa yana mahitaji makubwa duniani,”amesema
Amesema wapo katika hatua za mwisho kukamilisha mkakati huu maalum wa madini mkakati na muhimu ambao pia ni sehemu ya Kampeni ya Dunia katika kupunguza hewa ya ukaa kupitia matumizi ya nishati safi.
Akizungumza katika Mkutano huo Balozi wa Uingereza nchini Tanzania,Marriane Young amesema Uingereza inapongeza jitihada kubwa za kukuza sekta ya madini zinazofanywa na serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuahidi kuimarisha ushirikiano mkubwa baina ya nchi hizi hasa katika kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo kupitia Taasisi za madini nchini Uingereza na Tanzania.
Balozi Young ameunga mkono mpango wa uongezaji thamani madini nchini na kuahidi kwamba Uingereza itashirikiana na Tanzania kwa ukaribu ili malengo hayo yatimie.
More Stories
LALJI yatoa msaada wa sare na vifaa vya shule kwa yatima
Dkt.Biteko aagiza Kituo cha huduma kwa wateja Tanesco kusukwa upya
Rais Samia aridhishwa na uongozi safi wa Mwinyi