Na Penina Malundo,Timesmajira
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt. Suleiman Jafo amewataka Watanzania kuthamini bidhaa zinazotengenezwa nchini kwa lengo la kuongeza soko la ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa nchi.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa muonekano mpya wa juisi ya Afrikan Fruti inayozalishwa na Kampuni ya Bakhresa Food Products(BFPL),alisema ni vema kuthamini bidhaa zinazotengenezwa nchini kwani ni uzalendo.
Amesema bidhaa zinazotengenezwa nchini zikikosa soko na ajira kwa vijana zitapunguza kasi za ajira huku kusababisha uchumi wa nchi ukizorota.
“Mimi ni kawaida yangu nikienda ‘super market’ ni lazima ninunue bidhaa inayotengenezwa nchini kwangu kwa sababu najua ununuaji wangu unasaidia mambo mengi ikiwemo kuimarisha soko la ajira, kuongeza uchumi wan chi na hata kumsaidia muuzaji kuweza kutoa kodi yake kwa wakati.
Dkt. Jafo amesema Serikali inajitahidi kujenga miundombinu mizuri ya usafiri ili wafanyabiashara wapate urahisi wa kusafirisha bidhaa zao kwenda kila eneo analohitaji.
“Kila bidhaa inayosafirishwa nchini ni lazima isafirishwe ndio maana serikali imejitahidi kuwepo kwa usafiri wa Treni ya kisasa ya( SGR ) lengo ni kumrahisishia mfanyabiashara kusafirisha bidhaa yake,”amesema.
Aliupongeza uongozi wa Makampuni ya Bakheresa kwa kubuni bidhaa mbalimbali nchini na kuzalisha bidhaa zenye ubora.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya Bakhresa Food Products Ltd (BFPL) Salim Aziz amesema wamefanya uwekezaji nchini na nje ya mipaka ya nchi kwa lengo la kuipatia jamii huduma bora na kuliongezea pato taifa kutokana na kodi wanazolipa.
Aziz amesema kampuni hiyo inajishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za chakula, vinywaji,usafirishaji na burudani.
Amesema kampuni hiyo imewekeza viwanda 17 nchini ambavyo vyote vimetoa kipaumbele cha kuwaajiri wazawa wa ndani.
Akizungumzia kampuni ya Bakhresa Food Product LTD amesema ina jumla ya ya viwanda saba vinavyozalisha bidhaa za soda,maji safi,juisi ya matunda, ice cream na usindikaji wa matunda ghafi .
Amesema kampuni hiyo mwaka uliopita ilichangia kulipa kodi kiasi cha sh. bilioni 180 na wanatarajia mwaka huu watalipa zaidi ya bilioni 200.
Aziz amesema kampuni hiyo imetoa ajira za moja kwa moja kwa wafanyakazi 2,000 huku ajira zisizo rasmi ni 30,000.
Amesema kampuni hiyo inasindika matunda zaidi ya tani 45,000 kwa mwaka yenye thamani ya zaidi ya bilioni 25 hivyo wanatoa soko kwa wakulima wa matunda zaidi ya 150,000 nchini.
More Stories
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais
NIDA yawakumbusha wananchi kuchukua vitambulisho vyao