December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO inathamini mchango wa wadau wa maendeleo

📌 Aeleza faida za Tanzania kufanya biashara katika soko la EAPP na SAPP

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mha. Gissima Nyamo-Hanga,amesema shirika hilo linathamini michango inayotolewa na wadau wa maendeleo katika kuimarisha sekta ya nishati nchini.

Mha. Nyamo-Hanga ameyasema hayo Mombasa nchini Kenya,wakati akiwasilisha mada kuhusu Sekta ya Umeme Tanzania,katika mkutano uliowakutanisha nchi Wanachama wa Mashariki mwa Afirka (EAPP) na wadau mbalimbali katika sekta ya umeme.

“Tunatambua ushiriki wa wadau wa mendeleo katika kuongeza biashara ya umeme nchini Tanzania, kwa kufadhili miundombinu ya mfumo wa umeme katika maeneo ya uzalishaji na mifumo ya uambazaji wa umeme,”amesema Mha. Nyamo-Hanga.

Mha. Nyamo-Hanga amesema, kwa upande wa uzalishaji umeme wapo wawekezaji huku kukiwa hakuna wawekezaji binafsi kwa upande wa usambazaji wa umeme na kwa upande wa mfumo wa usafirishaji wa umeme unaendeshwa na Serikali kupitia TANESCO.

Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kuangalia njia bora ya kushirikisha sekta binafsi katika ujenzi na uendeshaji wa mifumo ya usafirishaji wa umeme bila kuathiri uthabiti wa mifumo hiyo.

Akielezea faida zitakazopatikana kutokana na Tanzania kushiriki soko la Kanda la biashara ya umeme kwa kuingia katika muunganiko wa kuuziana na kununua umeme kwa upande wa Mashariki (EAPP) na Kusini mwa Afrika (SAPP), Mha. Nyamo-Hanga amesema nchi itafaidika kwa kuuza umeme kutokana na uwekezaji mkubwa Serikali inaoufanya katika eneo la uzalishaji wa umeme.

Amesema kijiografia Tanzania ipo katikati,nchi zilizo upande wa Kaskazini mwa Afirika zitakapo hitaji kufanya biashara ya umeme na nchi zilizo Kusini mwa Afrika,zitalazimika kuupitisha umeme katika miundombinu ya kusafirishia umeme ya Tanzania hivyo Nchi itafaidika kwa kupata fedha za kigeni.

Amesema pia kwa upande mwingine kutakuwa na utulivu wa gridi kupitia kuunganishwa kwa gridi ya Kanda kwa karibu. Gridi ya kanda inayounganishwa itatoa fursa ya kuingiza nishati mbadala kutokana na akiba ya pamoja ya mifumo, kuongezeka kwa usalama wa ugavi wa umeme na fursa za kuuza/kununua umeme wa bei nafuu kutoka soko la Kanda.