Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),imeonesha kuridhishwa na hatua zilizofikiwa katika uendelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme wa jotoardhi kwenye maeneo ya Ngozi (MW 70) na Kyejo-Mbaka (MW 60).
Hayo yamebainishwa Desemba 10,2024, wakati wa ziara ilioongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA,Prof. Mark Mwandosy,ambayo imelenga kuona hatua iliyofikiwa katika uendelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Prof. Mwandosya,amesisitiza umuhimu wa kupanua wigo wa vyanzo vya kuzalisha umeme ikiwemo jotoardhi,ili kuboresha upatikanaji wa huduma za nishati kwa wananchi.
“Nishati ni injini ya maendeleo, na tuna kila sababu ya kutumia rasilimali tulizo nazo kwa ufanisi,ili wananchi wapate nishati kwa gharama nafuu,”amesema Prof. Mwandosya.
Aidha, Prof. Mwandosya ameipongeza kampuni ya Maendeleo ya Jotoardhi Tanzania (TGDC) kwa juhudi zake za kuhakikisha miradi hiyo inasonga mbele. Ambapo amelezea kufurahishwa na msukumo uliopo katika kuendeleza rasilimali watu kupitia mafunzo akisema kuwa juhudi hizo ni muhimu kwa ustawi wa sekta ya nishati nchini.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Umeme wa EWURA, Aurea Bigirwamungu, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa EWURA,amesisitiza kuwa dhamira ni kushirikiana na wadau wote kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa mafanikio.
Miradi ya jotoardhi ya Ngozi, Kyejo-Mbaka na Songwe inatarajiwa kuongeza uzalishaji wa nishati safi na ya gharama nafuu, huku ikiwanufaisha wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam