November 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania,Italia kushirikiana katika Utalii

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM

TANZANIA kupitia Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) na Italia kupitia Taasisi ya ENAIP – Veneto Impresa Sociale ya Italia zimesaini,hati ya makubaliano,lengo ni kuongeza ubora wa mafunzo kwa vitendo katika eneo la ukarimu na utalii.

Hafla ya kusaini makubaliano hayo imefanyika Novemba 19,2024 katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam ikishuhudiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii,Balozi, Dkt. Pindi Chana.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana,amesema makubaliano hayo ni muhimu kwa Taifa, yatawajengea uwezo walimu, wanafunzi na menejimenti ya NCT katika aina mbalimbali za vyakula, lugha, suala la ukarimu kwa wageni na utalii.

“Kipaumbele chetu ni kuongeza idadi ya watalii kutoka mataifa yote duniani ikiwemo soko la Italia,makubaliano haya ni moja ya mkakati wa kutoa huduma bora kwa watalii na hatimaye kuongeza idadi ya watalii nchini,”amesema Balozi Chana.

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Florian Mtey,amesema makubaliano hayo yatasaidia ukuzaji na utekelezaji wa mitaala katika nyanja za ukarimu na utalii, kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu za kufundisha ukarimu, na usimamizi wa vyuo vya utalii na ukarimu.

“Juhudi hizi za ushirikiano zitaimarisha kwa kiasi kikubwa utoaji wa mafunzo katika sekta ya utalii na ukarimu, na hivyo kuchangia ukuaji wa sekta hiyo, ambayo inabakia kuwa kipaumbele katika uchumi wa nchi yetu” amesema Dkt. Mtey.

Kwa upande wake, Balozi wa Italia nchini Tanzania, Giuseppe Sean Coppola, amesema kubadilishana uzoefu baina ya nchi hizo mbili ni muhimu katika kukuza Sekta ya Utalii ambayo ni sekta muhimu kwa maendeleo ya Taifa.