November 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mageuzi yanayofanywa na Rais Samia kwa mashirika ya umma kuongeza tija

Na Mwandishi Wetu, Arusha

MWAKA huu mkoani Arusha kilifanyika kikao kazi cha siku tatu, ambacho kiliandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kwa lengo la kuwaweka pamoja wakuu hao na kujadili mambo mbalimbali .

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja maboresho yanayoendelea katika kuimarisha usimamizi, uendeshaji na utendaji wa Taasisi za umma sambamba na kubadilishana uzoefu.

Kikao hicho ambacho kilifunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kilihudhuriwa na washiriki wanaotoka katika Mashirika ya Umma 248 ambayo yanamilikiwa na Serikali kwa silimia 100 na wengine wanatoka katika Mshirika 58 ambayo Serikali inamiliki hisa hadi asilimia 50.

Uzito wa kikao hicho kilichokuwa kinagusa uchumi wa nchi kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali unaozidi trilioni 76 ni moja ya sababu zilizomfanya Rais Samia kukipa uzito kikao na kuamua kuhudhuria na kutoa maelekezo ambayo yataongeza ufanisi wa mashirika hayo.

Katika Kikao hicho, Rais Samia , aliweka wazi uamuzi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kufuta na kuchanganya baadhi ya mashirika ambayo hayaonekani kufanya vizuri, uamuzi ambao ulisababisha kelele nyingi.

Kwa mujibu wa Rais Samia jambo hilo linasababishwa na watu kuogopa mageuzi yanayofanyika katika mashirika ya umma licha ya kuonekana kufanya vizuri katika baadhi ya maeneo.

Rais Samia alitoa mfano wa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) ambalo amesema tangu anaanza kazi mwaka 1977 amekuwa akilisikia.

“Wakati huo lilikuwa likizalisha betri za redio zilizokuwa zikijulikana ‘National’ baadaye lilizalisha mipira ya magari inaitwa gereral tires , lakini tangu hapo halikuwahi kusikika tena.

Kuanzia hapo, general tire ikafa kabisa, bwana ametoa bwana ametwaa na NDC haijulikani kama ipo au imekufa kwani kila mradi wake ni sifuri,” alisema.

Rais Samia aliongeza kusema, “Sijui ana mradi gani, hakuna. Sijui ana chuma Liganga, Mchuchuma hakuna. Sasa unajiuliza huyu anafanya kazi gani, lakini lilipokuja pendekezo huyu sasa aondoshwe wizara imeandika mabarua kila sehemu NDC yetu, haiwezi kufutwa.”

Alisema inawezekana malengo yaliyokuwa yamewekwa juu ya NDC yalikuwa mazuri ila huenda yamepitwa na wakati, hivyo yanahitaji yarekebishwe au haina kazi.

Alisema kwa sasa upo ushirikiano wa Taasisi za Umma na Binafsi (PPP) ambao huenda umechukua kazi za NDC, lakini kufutwa kwake kunajenga hofu ambayo wakati mwingine isiyokuwa na ulazima.

Alitoa mfano wa mashirika yaliyochanganywa na kutengeneza kitu kimoja ni Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) ambayo iliundwa kutokana na kuunganishwa taasisi ya utafiti ya viuatilifu vya kitropiki na kitengo cha huduma za afya za mimea ambazo zilikuwa zikifanya kazi zinazokaribiana na hayakuwa yanaleta faida.

“Kuchanganywa kwake sasa lile shirika lililoundwa (TPHPA) limeiwezesha Tanzania kupata vyeti vya ubora wa kimataifa kwa sababu malengo yote yamekusanywa na kufanya kazi moja na kukaa katika mlengo ambao ulitakiwa kufanyiwa kazi, sasa Tanzania ina viwango vya ubora wa kimataifa,” alisema.

Alisema kupatikana kwa vyeti hivyo vya ubora kumefanya kazi za Tanzania kutambuliwa kimataifa, masoko hayatakimbia bidhaa za Tanzania na wameweza kukusanya fedha na kutoa gawio serikalini. Amesema jambo hilo linathibitisha kuwapo faida ya kuchanganya mashirika ambayo hayafanyi vizuri huenda malengo yao yanafanana au yamepitwa na wakati.

“Kufuta pia si vibaya, kama uliundwa huko nyuma, haiui mtu jamani ambaye anazaliwa, anakua, anatumika, anatumika wee…Mpaka anakua basi Mungu anasema basi anamchukua.

Sasa itakuwa shirika tuliloliunda wenyewe kama halifanyi vizuri basi liondoke tu, hatuwezi kwenda kulinda nafasi za watu na mashirika hayazalishi, hayana tija haiwezekani,” alisema.
Alisema madhumuni ya Serikali ni mashirika yafanye kazi na kuzalisha, akitoa mfano wa yale yanayotoka nje ya nchi namna ambavyo yamekuwa yakichukua zabuni ikiwemo za kujenga, biashara na kukusanya fedha kwenda nchini kwao.

Sisi mashirika yetu yako hapahapa ndani, tunawapa nafas wale, wabebe fedha zetu wapeleke kwao sisi tunaangalia tu, kwa hiyo nadhani wakati umefika wa kubadilika na kubadilika kweli kweli,” alisema.

Rais Samia alisema kuna baadhi ya taasisi na mashirika ambayo yakitekeleza wajibu wake ipasavyo yatasaidia kuvutia wawekezaji wa nje ya nchi na kuboresha mashirika ya ndani ili yaweze kufanya uzalishaji mzuri.

Aidha, Rais Samia anataka mashirika kubadilika. Alitolea mfano Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuwa endapo litakuwa makini na kusimamia viwango vya uzalishaji wa ndani itawafanya wazalishaji wa ndani kufikia viwango vya kimataifa, hivyo kusaidia kuzuia bidhaa zilizo chini ya kiwango kuingia nchini.

Nyingine ni Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) ambao wakiweza kuwapa njia waliofikia uzalishaji wa bidhaa kwa viwango vya kimataifa namna ya kwenda kwenye masoko ya nje, hiyo itasaidia wawekezaji wa ndani.

“TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kwa mfano wakifanya kazi yao vizuri sana kuwafanya wawekezaji wanaofanya kazi nje kuja ndani, walipe viwango ambavyo havileti malalamiko, hakuna kuchukua mashine za watu, hakuna kubambika, tutavuta wawekezaji wengi waje kuwekeza,” alisema.

Aidha, Rais Samia, alitumia fursa ya kikao hicho kuwataka watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma nchini kumwambia ukweli hasa pindi anapowataka wawekeze sehemu ambayo wanaona haiwezi kuwa na tija.

Alisema kabla ya kufanya hivyo ni muhimu kufanyika tafiti na kujiridhisha kabla ya kuweka fedha.

Kwa mujibu wa Rais Samia ni muhimu kufanyika utafiti wa kutosha kabla ya kuamua kuwekeza, ili kupunguza hasara ambazo zinaweza kujitokeza pale Serikali inapowekeza katika miradi mbalimbali na kulinda rasilimali za wananchi.

Alitolea mfano wa uwekezaji katika mradi wa kwanza wa Mkulazi mkoani Morogoro ambao ulishindwa kutekelezwa chini ya Mtendaji Mkuu wa Shirika la Taifa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba.

“Mfano mbaya wa Mshomba alipowekeza kwenye Mkulanzi one, limradi likubwa hilo namuuliza ulikuwa na upembuzi yakinifu anasema ilikuwepo mheshimiwa. Nikamuuliza hukuona kwamba mradi mkubwa, aaah najua lakini ndiyo ilikuwa ‘wakati ule’.

“Lakini sasa kama kitu hakikupi faida unawekeza tu kwa sababu ya ‘wakati ule’, haiwezekani, nikamwambia hata nikikuita mimi nikikwambia wekeza pale ukiona pana hasara niambie mheshimiwa Rais pale kuna hasara usiingie, muwekeze mkiwa na uhakika fedha iliyowekezwa itarudi,” aalisisitiza Rais Samia.

Alisema yapo mashirika yenye utashi wa kisiasa na wengine wameingiza fedha sehemu ambazo hazitarudi.

“Sina kigugumizi kusema na nalisema hili sijui mara ya pili au tatu, mfano wangu mkubwa ni kama Ubungo Plaza, ilivyofunguliwa ilikuwa mikutano yote tunaswagwa huko, sasa hivi nani anatumia Ubungo Plaza,” alihoji.

Uwekezaji mwingine alioutolea mfano ni wa Benjamin Mkapa Tower na kumtaka Msajili wa Hazina kuwapeleka watendaji hao wakaone jengo hilo linavyotumika na kuwa tangu lilivyokuwa jipya halikuwahi kujaa.

“Katazameni uwekezaji kama ule, muwekeze mkiwa mna hakika fedha inayoingizwa itarudi, sekta binafsi akiweka shilingi yake ameshafanya utafiti wa kutosha.

Natoa mifano simlaumu mtu, hivyo kama hamuwezi wapeni sekta binafsi au wauzieni,” alisema.

Aidha, Rais Samia aliihimiza mashirika na za umma kuwekeza katika maeneo ya kimkakati akitolea mfano wa eneo la usalama wa chakula. Rais Samia alitolea mfano akiwa kwenye ziara mkoani Morogoro, alipozindua kiwanda cha sukari Mkulazi cha kampuni Hodhi ya Mkulazi (MHCL), chenye wana hisa wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Jeshi la Magereza Kupitia Shirika la Uzalishaji Mali (Shima).

Alisema NSSF na Magereza wamewekeza kimkakati na wameweza kufanikiwa baada ya mageuzi kadhaa ambapo awali mradi huo ulikwama kutekelezwa. Alieeleza mwanzoni mwa mwaka huu kulitokea uhaba wa sukari, eneo ambalo limewekezwa na sekta binafsi licha ya kutekeleza sera za Serikali ila wana mikakati yao wenyewe.

“Unaweza kuwa na uhaba wa kitu na usiwe na cha kufanya, tuliagiza nje ya wao na kujaza sukari kwenye nchi ili imfikie mnyonge na bei ya sukari ikashuka, lakini kile kimeudhi wenzetu..

Ila unajiuliza huyu mwekezaji Mtanzania kwa nini alifanya hivi mjombaake kijijini akanunue kilo kwa sh. 6,000 au 8,000 kwa kuangalia faida ya kiwanda chake.

Lakini tukiwa na wawekezaji mashirika ya umma kama hao wa Morogoro tukipata mikiki ya sekta binafsi, sukari inayozalishwa na shirika la umma itasaidia,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Umma, Augustino Vuma, alitoa rai kwa taasisi ambazo hazifanyi vizuri kujitafakari na kuona ambavyo zinaweza kubadilika na kufanya vizuri zaidi ili tija ya uwekezaji wa mitaji ya umma iweze kuonekana.

Alisema kwa uzoefu waliona kama Kamati zipo sababu kama nne kubwa ambazo zinafanya taasisi zisifanye vizuri, moja ni ukosefu wa mitaji, ambapo kuna taasisi ambazo hazina mitaji ya kutosha na wakati mwingine zinakosa mitaji kutokana na madeni makubwa ambayo Serikali inakuwa nayo.

“Yaani Serikali inakwenda kukopa huduma kwenye taasisi hizo, lakini hailipi kwa wakati mfano mzuri ni taasisi ya Bohari ya Dawa ( MSD), Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) wa na TIB,” alisema Vuma.

Alisema kwa mtazamo wao taasisi hizo zikiwezeshwa vizuri hasa kwa Serikali kulipa madeni yake ambayo inadaiwa na taasisi hizi zinaweza kufanya vizuri na zikaleta maendeleo makubwa kwenye maendeleo ya nchi yetu.

Aidha, Vua alisema tatizo lingine ni uwezo mdogo wa viongozi , kwani kuna viongozi wengine wanakwenda kwenye kamati tunavyokwenda nao kwenye majadiliano unaona kabisa uwezo wao ni wa kawaida sana na pengine inatokana na upatikanaji wao sio wa kiushundani.

Alitaja sababu ya tatu kuwa ni ukosefu nidhamu, mtu anafanya kosa hawajibishwe kwa namna yoyote na mwisho ni minyororo ya kiutendaji hasa upande wa ajira na upande wa manunuzi .

“Unaweza kupata ntendaji mzuri sana wa taasisi, lakini wale kule anaowakuta hata akitaka kuwabadilisha kwa sababu uwezo wao ni mdogo mchakato wake unakuwa ni mgumu sana.

“Lakini kwa upande wa manunuzi akitaka kufanya manunuzi anakuta mchakato mrefu tofauti na sekta binafsi ambao ni mfupi,” alisema na kuongeza mwarobaini wa hayo ni sheria mpya ya uwekezaji ambapo kutakuwa na mfuko wa uwekezaji ambao utakuwa unatoa mitaji.