November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Safari ya Dkt.Angeline kwenye siasa baada ya kuacha kazi-sehemu ya mwisho

Judith Ferdinand

Siku iliopita  tuliishia Dkt.Angeline anavyofurahia namna anavyo watumikia wananchi katika nafasi yake ya Ubunge jimboni Ilemela,na leo anasimulia mafanikio aliyoyapata katika nafasi hiyo

MAFANIKIO

Dkt.Angeline anasema, wakati anaingia kwenye uwakilishi wa wananchi kwa nafasi ya Ubunge mwaka 2015, Jimbo la Ilemela lilikuwa halijafunguka kimaendeleo,kulikuwa na barabara moja kubwa ya kwenda Airport.

Mtu akitaka kwenda Kayenze alilazimika kupita njia moja,akitaka kwenda Buswelu,akitokea Kirumba lazima azunguke apitie Wilaya ya Nyamagana, ukitaka kwenda Sangabuye  kutokea Buswelu,ulikuwa huwezi mpaka urudi barabara ya Airport ndio uendelee na safari.

“Sasa hivi Ilemela ni kama kijiji,kinafikika kila kona,naona tumepiga hatua. Kwa mara ya kwanza 2015-2020,tulifungua takribani kilomita 146 za barabara,ikiwemo ya Kahama-Isela kutokezea Kayenze kwa mzee Majdi. Kahama kwenda Ilalila,Igogwe,Isanzu unatokezea sekondari ya Sangabuye,Igogwe,Mwakilabela unakwenda Igombe,barabara ya Buswelu kwenda Shibula mpaka Tx imewekewa lami na inapitika,”.

Amina Masoud, mmoja wa wananchi wa mtaa wa Buteja, anasema Dkt. Angeline anajituma kama mwanaume, huku akifurahia huduma za maji, barabara, umeme, na kujengwa kwa zahanati mtaa wa Lukobe.

“Wananchi sasa wanaweza kusafiri kwa urahisi na kufika katikati ya mji, kupitia juhudi zake, mtaa umepata tenki kubwa la maji,tunajivunia kupata maji safi na salama,”.

Kada wa CCM Jimbo la Ilemela,Jumanne Baliana anasisitiza kuwa Dkt. Angeline ni mfano wa kuigwa, na mafanikio yake yanaonekana wazi kwani Jimbo la Ilemela lilikuwa halijafunguka.Awali walikuwa wanatumia nauli ya shilingi 5000,kufika Kayenze lakini sasa wanatumia shilingi 3000.

“Nikiwa msaidizi wake jimboni, niliiona kiu na hamu yake ya kuhakikisha kila jambo jema linawafikia wanailemela, ikiwemo kupambana  kuhakikisha kivuko cha Mv.Ilemela kinaundwa na kutia nanga Kayenze.Alipambana kutafuta saruji kwa ajili ya kuzalisha tofali  ambazo zimesaidia kunyanyua mabomba  katika miradi mbalimbali ilionzishwa na wananchi,”anaeleza Kazungu Safari aliyekuwa Katibu wa Mbunge Jimbo la Ilemela.

USHIRIKIANO WA WANANCHI

Dkt.Angeline ameimarisha demokrasia kwa kuanzisha mfumo wa ushirikiano kati yake na wananchi, ambapo wananchi wanashiriki katika uanzishwaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo, hii imeongeza uwazi na usimamizi mzuri wa rasilimali.

Anasema kupitia kauli mbiu ya “Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga” imekuwa mwongozo wa ushirikiano kati ya wananchi, Mbunge na serikali.

Amefanikiwa kutoa tofali zaidi ya 500,000,zimetumika kujenga madarasa,nyumba za ibada,ofisi za serikali za mitaa,chama na baadhi ya watu binafsi pamoja na uzio kwa baadhi ya shule.

Kati ya tofali hizo Mtaa wa Lumala Mashariki tofali 2,000 kwa ajili ya ofisi ya serikali ya mtaa huo,tofali 2,000 ujenzi wa kituo cha polisi  mtaa wa Balyehele,ujenzi wa Zahanati Mtaa wa Bwiru Press tofali 5,000.

Pia aliunga mkono  ujenzi wa Kanisa la AICT Mhonze  kwa kuchangia tofali takribani 3,500 nas shule ya msingi Umoja alichangia tofali 3,500.

“Haya yote yamefanyika siyo kwa Mfuko wa Jimbo pekee ambao kwa mwaka tunapata milioni 83.76, zipo fedha zangu binafsi, na nyingine zinazotokana na taasisi ya  The Angeline,ambayo imekuwa  kiunganishi (link), ya wadau wanaonisaidia katika shughuli za maendeleo wakiwemo Mwanza Huduma,Twiga Cement,Tanga Cement, ambao walinipa maroli ya saruji,iliotumika kufyatulia tofali kwa ajili ya shughuli za maendeleo.”

Mwenyekiti wa Mtaa wa Buteja, Kata ya Kahama, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Mabele Elias, anaeleza kuwa Dkt. Angeline amefanikisha demokrasia kwa kuwezesha wananchi kushiriki katika miradi, ambapo bila yeye, maendeleo yasingewezekana.

“Wananchi tumeanzisha mradi kwa kujenga msingi, Mbunge anatoa tofali kwa ajili ya miradi mbalimbali.Kata ya Kahama ametoa tofali kwa shule za msingi ikiwemo Kahama,Buyombe na Magaka huku shule za sekondari ni Luguka na Lukobe.Wananchi wameshiriki katika miradi kwa michango yao na nguvu kazi,”anaeleza Mabele.

“Mpango wake wa maendeleo ya Ilemela,umekuwa na mafanikio, jamii inashirikiana kwa ukaribu,shule ya msingi Lukobe,wananchi tulijenga msingi,sasa ina boma ambalo limejengwa kutokana na tofali alizotoa Dkt.Angeline,”anaeleza Rebecca Elinzu,mmoja wa wanachi wa mtaa wa Buteja.

Ofisa Elimu,Vifaa na Takwimu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Johannes John,anaeleza kuwa Mbunge huyo wa Jimbo la Ilemela,kupitia Mfuko wa Jimbo ametoa fedha,ambazo zimetumika kujenga baadhi ya madarasa.Pia amesaidia kutengeneza tofali nyingi kupitia taasisi ya The Angeline.Madarasa takribani 49,yamejengwa kwa utaratibu wa wananchi kujenga msingi,Mbunge kutoa tofali za kunyanyua boma na halmashauri kumalizia.

HAKI ZA MAKUNDI MAALUM

“Nimefanikiwa kuwarudisha watoto wa kike zaidi ya  50 shuleni, waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali kama mimba.Kila Kata tulianza kuwachukua watoto wawili wawili,tukawapeleka Chuo cha Maendeleo Malya,na wengine waliendelea na masomo yao wakiwa na watoto wao,wengine wamemaliza na wanaendelea na maisha yao,”anaeleza Dkt.Angeline.

Jumanne Baliana, anasisitiza kuwa, Dkt.Angeline amekuwa akipinga vitendo vya ukatili ambapo amewezesha  pikipiki kwa SMAUJATA, kwa ajili ya kuwarahisishia usafiri wa kwenda kutatua changamoto ya vitendo vya ukatili jimboni Ilemela.

MICHEZO, AJIRA KWA VIJANA

Dkt. Angeline amekuwa akifanya mashindano ya The Angeline Jimbo Cup,mara nane mfululizo tangu  mwaka 2016 mpaka sasa,yameweza kuibua vipaji vipya na kuwapatia ajira vijana zaidi ya  10, walichukuliwa na timu kubwa wakiwemo watano wanaochezea timu za nje kama Kelvin John,wengine wamaechukuliwa na  timu za Simba Sc, wengine timu za daraja la kwanza.Huku watano wapo Chuo cha michezo Malya.

“Lengo  ni kusaka vipaji kwa vijana na waweze kupata ajira kupitia michezo,wachangamshe akili,wasijiingize katika tabia na makundi hatarishi.Nitaendeleza mashindano hayo kwa kushirikiana na Chama cha soka Wilaya,ata nikiwa nimestaafu siasa,”anaeleza Dkt.Angeline

Kocha wa timu ya Kata ya Ibungilo,Deusdedith Bosco,anasema Dkt.Angeline  ni muhimu katika kuendeleza vipaji jimboni Ilemela kupitia The Angeline Jimbo Cup.

“Nina wachezaji watatu,waliopata nafasi katika timu kubwa kupitia mashindano haya  akiwemo Daniel Hapsen,aliyechukuliwa na Alliance FC,inayoshiriki ligi daraja la pili,wawili wamechukuliwa na timu ya Pamba Jiji kikosi cha chini ya miaka 20.Baadhi ya wachezaji wanaendelea kupokea ofa kutoka timu mbalimbali nchini,”.

Mmoja wa wadau wa soka wilayani Ilemela mkoani Mwanza,Shukrani Dickson, anasema mashindano ya Angeline Jimbo Cup,ni msingi wa kuibua vipaji na kutoa ajira kwa vijana,yameonesha dhamira ya kuendeleza michezo pia ni muhimu kwa maendeleo ya jamii.

“Dkt.Angeline ni mwanamke ambaye amethubutu,kuna baadhi ya majimbo yanaongozwa na wanaume,lakini hatuoni vitu kama hivi vya maendeleo yaliofanywa katika sekta ya michezo na sisis ndio wadau tunayaona haya kwa ukubwa,”anaeleza Shukrani.

Katibu wa Chama cha Soka Wilaya ya Ilemela (IDFA),Mratibu wa mashindano ya Angeline Jimbo Cup,Almas Moshi,anaeleza kuwa mashindano hayo yanachukua wachezaji ambao wapo chini kutoka kata 19 za jimboni Ilemela huku malengo yake yakifanikiwa kwa kiasi kikubwa.

“Baadhi ya wachezaji,walioibuliwa kupitia mashindano hayo wamepata ajira kwenye timu kubwa ndani na nje ya nchi,akiwemo Kelvin John  aliyewai kuichezea  klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji ambaye sasa amejiunga na club ya Alborg Fc ya nchini Denmark ,Kelvin Kijili timu ya Simba SC,Marko Saramba Pamba Jiji,Andrea Mengi timu ya Prison,Andrea Methew anachezea Kagera Sugar,”anaeleza Almas na kuongeza:

“Kupitia mashindano hayo upande wa wanawake wachezaji nane wameweza kupata timu  akiwemo Irene anayechezea timu ya wanawake chini ya miaka 17,akitokea Kata ya Kayenze,kwenye Jimbo Cup alikuwa anachezea timu ya TSC Academy,Sabina anachezea timu ya Yanga Princess,baada ya mashindano mwaka 2023 akapata usajili wa timu hiyo,”.

Almas anasema,Dkt.Angelinea anaendesha mashindano kupitia fedha zake na taasisi ya Angeline.Kila mwaka yamekuwa bora mwaka 2016 wakati yanaanza mshindi wa kwanza alipata zawadi ya milioni moja,wa pili laki tano  na watatu laki tatu.

“Msimu huu wa nane,zawadi zimekuwa bora na wigo umepanuka ambapo mwaka 2024,mshindi wa kwanza amepata milioni 2.5,wa pili milioni mbili,wa tatu milioni 1.5,pia tumekuwa na mshindi wa nne alijinyakulia kitita cha milioni moja,”.

KUTATUA MIGOGORO

Dkt. Angeline,anasimulia kuwa wakati akiwa Naibu Waziri, na Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,alifanikiwa kutatua migogoro ya ardhi kwa makundi,ikiwemo wa Polisi na wananchi,eneo la Kigoto Kata ya Kirumba ,kaya zaidi ya 600 zilirejeshewa eneo lao na kupatiwa hati.

Kata ya Kiseke eneo la Nsumba,eneo lilichukuliwa na Mkoa,kutokana na   kelele za wenyeji kwamba hawakuzingatiwa haki zao,walilirejesha kwa wananchi.Migogoro mingine aliofanikiwa kutatua ni wa Kata ya Ilemela kati ya Jeshi na wananchi,kaya zilikuwa nyingi na zililipwa takribani bilioni 6.

“Migogoro hii yote,niliikuta ina miaka  12 nyuma, nilijikita kushughulika  inayogusa watu wengi ya  mtu mmoja mmoja ni michache tuliwafikia kulingana na alivyokunja,na mingi ya Ilemela ni ile ambayo ardhi ilitwaliwa kabla ya mwaka 2000, ambako ardhi ilikuwa haina thamani mtu alikua analipwa muendelezo,”.

“Nikiwa Naibu Waziri,mpaka Waziri, Ilemela ilikuwa inaongozwa katika suala zima la utoaji wa hati,kwenye masuala ya urasimishaji Ilemela ilikuwa inaongoza mpaka leo tunafanya vizuri,lakini wanailemela wenyewe hawaoni,”.

Anasisitiza kuwa,suala la ardhi lina ugumu wake,kulisimamia lakini,linaurahisi pale  utakapokubali kusikiliza hoja na kujua sheria zinasema nini na unajua nini cha kufanya.

“Kwa kipindi changu ndio Rais aliridhia kupunguza nusu ya gharama ya umiliki wa ardhi.Kuanzia kwenye masuala ya hati kutoka kwenye shilingi 50,000, ikiwa shilingi 25,000.Pia alitoa msamaha kwa kodi za ardhi kwa wale waliokuwa na muda mrefu,”anaeleza na kuongeza:

“Kinachonipa furaha na ninajivunia wakati nikiwa  Waziri,nilianzisha kliniki ya ardhi,mwaka 2022, imesaidia kwa nchi nzima.Ambapo  wanakutana sehemu moja, wataalamu,wananchi wanatoa hoja zao,imesaidia watu kufikiwa kwa wakati na kutatuliwa kero zao,”.