Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Magharibi imewataka mafundi na wataalamu wa umeme kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa ili kuepusha hitilafu zinazoweza kusababisha athari na uharibifu.
Rai hiyo imetolewa jana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora (RAS) Dkt John Mboya alipokuwa akifungua semina ya siku moja kwa wadau, mafundi na wataalamu wa mifumo ya umeme iliyoandaliwa na EWURA Kanda ya Magharibi.
Amepongeza EWURA kwa kuandaa semina hiyo ili kuwezesha Wataalamu na Mafundi wote wanaojishughulisha na kazi za umeme kufanya kazi zao kwa kufuata taratibu na kwa ufanisi na weledi mkubwa.
Amesisitiza kuwa utaratibu uliowekwa na Mamlaka hiyo wa kutoa leseni kwa Mafundi na Wataalamu wote wanaofanya kazi hizo ni wa muhimu sana kwa kuwa utachochea weledi na kupunguza athari zitokanazo na mifumo mibaya ya umeme.
‘Kupitia semina hii ni marufuku kwa mafundi wasio na leseni za EWURA kufanya kazi yoyote ya kuunganishia wananchi umeme katika nyumba zao au majengo ya biashara, hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao’, amesema RAS.
Dkt Mboya amewataka watumiaji wa huduma za maji na vifaa vya nishati kuacha kutumia vifaa feki na mafundi wasio na leseni ili kuepuka athari zitokanazo na vifaa hivyo ikiwemo ufungaji mbovu wa mifumo ya umeme katika majengo yao.
Meneja wa Mamlaka hiyo Kanda ya Magharibi Mhandisi Walter Geofrey Christopher amesisitiza kuwa sheria inataka mafundi umeme wote kuhakikisha wana leseni za EWURA kinyume na hapo ni kosa kisheria na hatua zitachukuliwa.
Amebainisha hatua zinazoweza kuchukuliwa kwa Mafundi watakaofanya kazi ya kuunganisha mifumo ya umeme bila leseni kuwa ni kutozwa faini isiyopungua sh milioni 1 au kifungo cha miaka 5 au vyote kwa pamoja.
Amefafanua kuwa semina hiyo imelenga kuwajengea uelewa wa sheria na taratibu zinazoongoza kazi zao na kile kinachotakiwa kufanyika wakati wa utekelezaji kazi zao ikiwemo uandaaji michoro ya mfumo wa umeme katika majengo husika.
Mhandisi Christopher ameongeza kuwa kila fundi anatakiwa kuelewa aina ya mfumo wa umeme unaotakiwa katika jengo fulani kabla ya kuanza kazi, alionya kuwa atakayebainika kutumia mfumo usiokubalika atawajibika.
Naye Mwenyekiti wa Wakandarasi wa Umeme Mkoani hapa Mwinyi Mgumia ameeleza kuwa semina hiyo ni muhimu sana kwao kwa kuwa itamfanya kila mmoja kufanya kazi iliyo bora zaidi na mafundi wababaishaji (vishoka) watabainika.
Ameongeza kuwa mkakati wao ni kuendelea kuhamasisha mafundi wenzao kufanya kazi iliyo bora zaidi ikiwemo kuhakikisha wote wanakuwa na leseni za EWURA ili wafanye kazi zao kwa uhuru.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi