September 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake, vijana watakiwa kuchangamkia fursa za zabuni

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Wanawake na Vijana nchini wametakiwa kuchangamkia fursa za zabuni zilizopo serikalini kwa kujisajili katika mfumo wa usimamizi wa ununuzi (NeST) unaopatikana kupitia simu janja.

Hayo yalisemwa jana na Meneja wa Kanda ya Pwani- PPRA, Vicky Mollel katika mafunzo ya siku tatu yaliyoanza Septemba 17-19 mwaka huu kuhusu mradi wa uwezeshaji wanawake na vijana kushiriki katika manunuzi ya Umma (BID FOR SUCCESS) yaliyoandaliwa na Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC ) na Trade mark Afrika kwa kushirkiana na wawezeshaji kutoka Tenderbank.

Mollel alisema PPRA kwa kushirikiana na TWCC wanawawezesha wanawake kuweza kujua fursa zilizopo ili waweze kuzichangamkia fursa hizo.

“Katika sheria ya ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 imeweka fursa nyingi kwaajili ya kuwainua watanzania wakiwemo makundi maalum ambapo tassisi nunuzi inatakiwa kutenga asilimia 30 ya bajeti yake ya ununuzi kwaajili ya makundi hayo yanayohusisha wanawake , vijana, wazee na watu wenye ulemavu”

“Katika fursa ya makundi haya maalum kipengele cha uzoefu hakitaangaliwa sana kwani kuna kazi ambazo zitatolewa tu kwa lengo la kuwainua wanawake au watanzania”

Mollel alizitaja changamoto zinazowakumba wanawake wanaoshindwa kuchangamkia fursa hizo ikiwa ni pamoja na kutozifahamu fursa zenyewe kwa undani zaidi.

“Changamoto zilizopo kwa wanawake ni kutokufahamu fursa zilizopo kwamba kuna wengine bado wanafikiria masuala ya connection au kujuana ambapo mtu anakua na biashara yake badala ya kuchangamkia fursa ya kujiunga kwenye mfumo na fursa zinazotangazwa kila siku na taasiis nunuzi bado wana masuala ya kujuana”

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi huo, Julieth Sandi alisema Mradi huo ni wa miaka mitatu kutoka mwaka 2024-2027 umelenga kuwafikia wanawake na vijana zaidi ya 1000 Tanzania nzima

Alisema pamoja na kwamba mradi huo upo Katika awamu ya pili, watafany mafunzo kwa awamu ya tatu, nne na tano ambapo awamu mbili zitafanyika katika Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kati Dodoma huku akiwahimiza wanawake na vijana wengi zaidi kushiriki katika mradi huo kwani kundi hilo
Limeonekana kukosa uelewa wa kutosha kwenye fursa zilizopo kwenye manunuzi.

“Wanawake wengi wanahimizwa kushirki ni kutokana na kwamba wanawake wengi na vijana hasa waliopo katika hili kundi ambalo linaonekana halishiriki sana kwenye masuala ya tenda wanakosa uelewa na hawajapata elimu ya kutosha kwenye fursa mbalimbali ambazo zipo kwenye manunuzi ya umma na mashirika binafsi”

“Wanawake wengi wapo wanabiashara nzuri na zinafanya vizuri lakini hawajaweza kuthubutu na inawezekana kutokana na kutopata elimu sahihi, hivyo mradi huu unawaonesha kwamba kuna fursa mbalimbali ambazo wanawake na vijana na wenye ulemavu wanaweza wakazipata ili kuweza kuzifanikisha bidhaa zao”

Naye Mfanyabiashara wa Chakula kutoka mkoa wa Lindi, Noela Lukanga mafunzo hayo yamewasaidia wanawake wafanyabiashara namna ya kupiga hatua katika biashara zao za kila siku hivyo aliwataka wanawake na vijana wote kuendelea kuzingatia mafunzo hayo ili kujipatia fursa mbalimbali na kuweza kujikwamua
Kiuchumi.

Mratibu wa Masoko na Mauzo kutoka kutoka kampuni ha Wiznet Enterprises Said Yahaya alisema mafunzo hayo yamewasaidia kupata njia za kuweza kujiajiri na kuweza kujiinua kiuchumi hivyo aliwataka vijana wengine kuweza kushiriki katika mafunzo hayo ili kuweza kupata maarifa kuhusu mamunuzi.