November 9, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uchaguzi Serikali Mtaa waiva, Vijiji 12,333, Vitongoji 64,274, Mitaa 4,269 Kuhusika.

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa ametangaza jumla ya Vijiji 12,333, Mitaa 4,269 na Vitongoji 64,274 kuwa vitashiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha Jumatatu Septemba 16, 2024 kwenye Ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mchengerwa amewaambia wanahabari kuwa orodha hiyo imejumuisha maeneo yaliyokuwa yamefutwa awali kwa mujibu wa tangazo la serikali ambayo pia yalihusisha Tarafa ya Ngorongoro mkoani Arusha.

Mchengerwa amesema Notisi ya mgawanyo wa maeneo ya Utawala katika Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Tangazo la Serikali namba 769 la mwaka 2024, limetolewa kwa mujibu wa vifungu vya 16(1) na 18(1) vya Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288

Amesema tangazo hilo limebainisha mipaka ya vijiji, mitaa na vitongoji vitakavyohusika katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 na pia tangazo hilo limerejesha vijiji vya Ngorongoro vilivyofutwa kwa tangazo la Serikali namba 673 na Tangazo la Serikali namba 674 la Agosti 02,2024.

Aidha Mchengerwa amewataka Watanzania kujiorodhesha katika orodha ya wapiga kura kati ya Oktoba 11 hadi Oktoba 20,2024 na pia kujindaa katika kugombea nafasi mbalimbali za Uongozi katika uchaguzi utakaofanyika Novemba 27,2024.

“Ofisi ya Rais Tamisemi imejiandaa vyema kuhakikisha kwamba uchaguzi huu unakuwa huru na wa haki katika misingi ya 4R kama ambavyo Mheshimiwa Rais ameendelea kusisitiza. Mchakato huu ni fursa kwa wananchi kushiriki moja kwa moja katika kuamua mustakabali wa maendeleo ya maeneo yao”amesema.