November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahitimu Chuo cha Pasiansi hazina adhimu kwa Sekta ya Maliasili,Utalii

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Sekta binafsi zinazojishughulisha na uhifadhi wa wanyamapori au biashara zinazoendana na uhifadhi wa wanyampori zimetakiwa kutoa nafasi za ajira kwa vijana waliohitimu katika Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi ili kuongeza tija katika shughuli za Uhifadhi na Utalii kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wanachi maendeleo kupitia Maliasili na Utalii.

Wito huo umetolewa kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula Jijini Mwanza, kwenye mahafali ya 59 ya Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi.

Kitandula amesema wahitimu wa mafunzo ya Uaskari wa Wanyamapori na Himasheria, Uongozaji na Usalama wa Watalii na mafunzo ya muda mfupi kwa askari wa vijiji kutoka maeneo mbalimbali ni hazina muhimu kwa Uhifadhi na Utalii hivyo ni vyema wakatumike vizuri kwa maslai mapana ya Taifa.

Aidha Kitandula ametumia fursa hiyo kuwapongeza na kuwashukuru wafadhili wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) kwa kulipia ada za masomo na mahitaji mengine kwa baadhi ya askari hao ili kufanikisha kuhitimu mafunzo .

Akitoa Taarifa ya Mafunzo hayo Mkuu wa Chuo hicho,Jeremiah Msigwa amefafanua kuwa kati ya wanachuo 374 waliodahiliwa,Wanachuo 354 wamepewa vyeti vya kuhitimu mafunzo kulingana na viwango (grade) mbalimbali vya ufaulu wakiwemo wanachuo 222 wa kozi ya BTCWLE, 70 wa kozi ya TCWLE; 34 wa kozi ya BTCTGTS na 04 wa kozi ya TCTGTS.