November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watu 12 wafariki 33 wajeruhiwa kwa ajali Mbeya,RC atoa maagizo

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline, Mbeya

WATU 12 wamefariki dunia na wengine 33 kujeruhiwa baada ya basi lenye namba za usajili T 282 CXT mali ya Kampuni ya A-N COACH lilokuwa likitokea Mbeya kuelekea Tabora kuacha kugonga gema kisha kupinduka na kusababisha vifo na majeruhi .

Kwa mujibu wa Kaimu kamanda wa Polisi Mbeya , Wilbert Siwa amesema tukio hilo limetokea septemba 6, mwaka huu majira ya saa 1.30 asubuhi katika eneo la Lwanjiro Wilaya ya Mbeya katika barabara ya Chunya .

Kamanda Siwa amesema miongoni mwa waliofariki ni pamoja na dereva wa basi hilo Hamduni Salum(37) mkazi wa Tabora huku ikielezwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi uliopelekea basi hilo kuacha njia na kupinduka.

Siwa amesema kati ya watu 12, waliopoteza maisha wanaume 5, wanawake 7, wakiwepo watoto wadogo ni wawili huku kati ya majeruhi 33 wanaume walikuwa 22 na wanawake 11 ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa kanda ya Mbeya,hospitali ya Wilaya ya Chunya na kituo cha afya Chalangwa.

Kamanda Siwa amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva kushindwa kulimudu gari lake kwenye eneo lenye mteremko na kona kali .

Amesema Jeshi la polisi linaendelea kutoa wito kwa madereva kuwa makini na kuzingatia sheria, alama na michoro ya usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Chunya Dkt.Darson Andrew amethibitisha kuwapokea Majeruhi na maiti 11 kati yao wanaume watano na Wanawake sita.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amesema kufuatia ajali hizo zilizotokea kwa nyakati tofauti Wilaya ya Chunya na Mbarali ameagiza kikosi cha usalama barabarani na Mamlaka ya Udhibiti wa usafiri wa ardhini(LATRA)kufanya ukaguzi wa mabasi ya abiria na yatakayobainika mabovu kuyafungua.

“Tayari nimetoa maelezo kwa mamlaka husika wakiwepo Polisi usalama barabarani,Latra hususan Wakala wa Barabara(TANROADS)kuweka alama kwenye maeneo yote hatarishi ili kudhibiti ajali za barabarani zisizo za lazima sambamba na ukaguzi wa mifumo ya VCT”amesema.

Homera amesema kuwa katika uchunguzi uliofanyika umebaini ajali iliyotokea Septemba 3,2024 katika kijiji cha Itamboleo kata ya Chimala na leo Septemba 6 mwaka huu zimebaini madereva wa vyombo vya moto waliondoa mifumo ya udhibiti mwendo (VCT) ambapo pia ameagiza mabasi yote yafanyiwe ukaguzi a kuzuiliwa kama hayajakidhi vigezo vya kuendelea na safari”amesema Homera.