Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora
MABORESHO makubwa ya miundombinu na utoaji huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora (Kitete) yamewezesha mapato kuongezeka kutoka sh mil 129 hadi mil 252 katika kipindi cha miezi 3 ya Juni, Julai na Agosti.
Hayo yameelezwa na Mganga Mfawidhi wa Hospital hiyo Dkt Joackim Eyembe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na Maafisa wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Magharibi waliotembelea hospitali hiyo jana.
Amebainisha kuwa mafanikio hayo yamepatikana kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kuboresha upatikanaji huduma za afya na dawa katika hospitali hiyo.
Amesema kuwa kwa sasa wanapata zaidi ya asilimia 90 ya mahitaji ya dawa zote kutoka Bohari ya Dawa (MSD) hali ambayo imepelekea kuboreshwa huduma za afya na wagonjwa wote wanaoletwa katika hospitali hiyo kupata huduma stahiki.
Dkt Eyembe ameongeza kuwa hospitali hiyo haina changamoto tena ya ukosefu wa dawa kama ilivyokuwa huko nyuma, wanapata dawa kwa wakati na zipo za kutosha na wameanzisha duka ili wananchi wasihangaike kwenda kununua nje.
Aidha ametaja maboresho mengine yaliyofanyika katika Hospitali hiyo kuwa ni kujengwa wodi mpya na kupatiwa vifaa vya kisasa na madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali ya binadamu.
Ametaja baadhi ya vifaa hivyo kuwa ni vitanda vya kisasa vilivyowekwa katika wodi ya akinamama wajawazito na watoto, mashine za kidigitali za mionzi (x-ray na ultra sound), vifaa hivyo vyote vimegharimu zaidi ya sh bilioni 2.
‘Tunawashukuru sana MSD kwa juhudi zao za dhati za kuhakikisha Vituo vyote vya Kutolea Huduma za Afya ikiwemo Hospitali za Wilaya na za Rufaa zinapata na dawa za kutosha, hili limechochea mapato yetu kuongezeka’, amesema.
Naye Kaimu Meneja wa Bohari ya Dawa Kanda ya Magharibi Rashid Omary ameeleza kuwa MSD itaendelea kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati katika Vituo vyote vya Kutolea Huduma na Hospitali zote ili wananchi wapate huduma.
Amebainisha kuwa ufanisi wa utoaji huduma katika hospitali hiyo umeboreshwa kutokana na kuwezeshwa dawa na vifaa tiba vya kutosha ikiwemo maboresho ya miundombinu yaliyofanywa na serikali ya awamu ya 6.
More Stories
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi