Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora
SERIKALI kupitia Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Magharibi imewahakikishia wakazi wa Mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi kuwa itaendelea kupeleka dawa za kutosha katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya ikiwemo Hospitali za Wilaya hata kama halmashauri hazina pesa za kulipia kwa wakati huo.
Hayo yamebainishwa jana na Kaimu Meneja wa MSD Kanda ya Magharibi Rashid Omari alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Mkoani hapa katika kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Bohari ya Dawa nchini.
Amesema kuwa huu ni mkakati wa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa zaidi ya asilimia 90 katika Kanda hiyo na maeneo mengine.
Ameongeza kuwa kupitia mkakati huu Bohari ya Dawa imejipanga kuhakikisha huduma za matibabu zinatolewa kikamilifu kwa jamii katika zahanati, vituo vya afya na Hospitali zote zilizo chini ya Halmashauri za wilaya.
Omari amefafanua kuwa serikali ya awamu ya 6 inajali sana wananchi ndiyo maana MSD imekuja na mpango mkakati wa kuhudumia wananchi kwanza maslahi ya fedha yatafuata baadae.
Amebainisha kuwa Rais Dkt Samia amefanya maboresho makubwa sana katika sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya ya kutosha, zahanati na hospitali za wilaya tofauti na kipindi cha nyuma ili kusogeza huduma za afya kwa wananchi.
Meneja huyo ambaye Kitaaluma ni Mfamasia ameongeza kuwa kwa sasa MSD inasambaza dawa mara 6 kwa mwaka ikiwa ni kila baada ya miezi 2 tofauti na zamani ambapo walikuwa wanasambaza dawa mara 4 kwa mwaka.
Ameeleza kuwa nia na madhumuni ya kasi hiyo ni kuimarisha upatikanaji dawa katika vituo vya afya vyote na kuboresha miundombinu ya ufikishaji dawa hizo katika Vituo vyote mahali popote.
‘Kwa sasa kila baada ya miezi 2 MSD inasambaza tani 40 hadi 50 za dawa wakati huko nyuma tulikuwa tunasambaza tani 5 hadi 10 kila baada ya miezi 6, haya ni mabadiliko makubwa sana’, amesema.
Awali Meneja Mawasiliano na Uhusiano MSD Etty Kusiluka ameeleza kuwa serikali imeendelea kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kusambaza dawa katika maeneo yote yenye Vituo vyote 8200 vya Kutolea huduma za afya nchini.
Amesema wamejipanga vizuri ili kuhakikisha inatoa zoezi la usamazaji dawa linafanyika kwa weledi mkubwa ili ziwafikie wananchi katika Kanda zote 10 zilizopo hapa nchini ikiwemo Kanda ya Magharibi.
Amebainisha kuwa MSD imejenga maghahala makubwa ya kuhifadhia dawa katika Mikoa ya Dodoma na Mtwara ili kurahisisha usambazaji dawa katika Mikoa yote nchini na kuwezesha wananchi kupata huduma bora za afya.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa