December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake watolewa dhana potofu kumiliki mashamba ya kahawa

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

IMEELEZWA kuwa Mila na desturi zilizopitwa na wakati zilikuwa zinajenga imani kwamba baadhi ya mazao hayastahili kwa wanawake kulimwa ikiwemo zao la kahawa ambapo awali mwanamke hakustahili kumiliki mashamba ya kahawa na baadhi ya mazao kutoliwa na wanawake.

Baadhi ya wanawake wameonyesha kushangazwa kwa wanawake wenzao kumiliki mashamba ya kahawa na kutokana na dhana iliyojengeka ya kudhani kuwa mashamba ya kahawa yanamilikiwa na wanaume pekee.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la MIICO linalofanya kazi kwa kushirikiana na Jukwaa la wanawake wa Vijijini Tanzania,Catherine Mulaga wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake kutoka mikoa ya Songwe na Mbeya  kuhusiana na mbegu za asili kwa wakulima waliopo Vijijini.

“Katika mafunzo haya wanawake wameonyesha haja  kubwa ya kutaka kuendeleza mbegu za asili baada ya kujifunza kutoka kwa wenzao,kitu kikubwa ambacho wamekipata katika kubadilishana uzoefu ni Mila na desturi ambazo zimepitwa na wakati ambapo Mila hizo zilijenga imani kuwa baadhi ya mazao hayastahili kwa wanawake au baadhi ya mazao hayaliwi na watu fulani ,mfano zao la kahawa baadhi ya wanawake wameshangaa kuona wanawake wenzao wanamiliki mashamba ya kahawa “amesema Mulaga.

Akielezea zaidi Mulaga amesema kitu kingine walichojifunza ni imani potofu iliyokuwepo kipindi cha nyuma juu ya baadhi ya mbegu ambazo sio sahihi kuendelea kuamini  kwamba  mbegu hizo zina faida katika lishe kwa watu ambapo inapaswa kuendelezwa na kuwa njia ya kuu ya kuendeleza mbegu za asili ni kubadilishana na kwenda kuzalisha na kuhifadhi kwa misingi inayotakiwa ili kuendelea kuzitumia na kuwafundisha watoto ili waweze kuzitambua kwa manufaa ya baadaye.

Aidha Mulaga ametoa wito kwa wanawake kulima zao la kahawa badala ya kuamini wanaume pekee ndo wanaweza kulima kilimo cha kahawa na kusema kuwa uzoefu inaonyesha kuwa  wanawake ni wasimamizi wazuri wa kwenye kilimo na umakini kuliko wanaume na wanawake waamini kwamba wanawaweza kuwa wakulima wazuri kwa kushirikiana na waume zao.

Mmoja wa wanawake walioshiriki mafunzo hayo katika ukumbi wa mikutano wa Ifisi halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Hawa  Mahanyu kutoka wilaya ya Mbozi Kijiji cha Mahenje mkoa wa Songwe amesema kwamba kipindi cha nyuma wanaume ndiyo walikuwa wakilima mashamba ya kahawa kukiwa na dhana kwamba kilimo hicho kilipaswa kulimwa na wanaume pekee na kusema kuwa baada ya kupata mafunzo kutoka Jukwaa la wanawake vijijini kuhusu jinsia na kilimo amegundua kilimo ni cha mwanaume  na mwanamke hakuna jinsia inayochagua.

“Nilichogundua ni kwamba kipindi cha nyuma wanaume wa Mbozi walikuwa na mfumo dume mwanamke kazi yake ilikuwa kulima mazao ya chakula ambayo ni Maharage,Mahindi ambapo wanaume walikuwa wakilima mashamba ya kahawa kama zao la kimkakati la biashara baada ya kupata mafunzo walifanya majaribio kuona kilimo cha kahawa kina kazi gani tulianza kushiriki kazi za kilimo kwenye mashamba yetu maana mwanamke hapo mwanzo alikuwa haingii kwenye mashamba ya kahawa kuanzia upandaji ,uvunaji,upigaji dawa mpaka uvunaji wa kahawa “amesema Mahanyu.

Aidha Mahanyu amesema kwamba baada ya hapo wakawashawishi wanaume kutoa maeneo kwa ajili ya kuchimba mashamba ya kahawa pamoja na watoto wa wakike ambapo katika shule ya  Sekondari ya Mnyovinzi ambao waliopatwa miche ya kahawa na kuendeleza.

Hata hivyo Mahanyu amefafanua kuwa walianza mfumo wa zao la kahawa waliona ni zao la kimkakati ambalo lina fedha kuliko mazao mengine yote na hakuna kazi yoyote endapo watazingatia kilimo na pia waliingia katika mafunzo ya kilimo Ikolojia kwa ajili ya kilimo cha kahawa na kwamba wengi wanadhani ni kuchakata kuongeza dhamani ni kutotumia madawa makali ili kuongeza ladha kwa kuhifadhi samadi baadaye inakuja kutumika kwenye mashamba ya kahawa.

Mahanyu ametoa wito kwa wanawake kwa kuona kuwa zao la kahawa ni gumu kwa kuona wanaume pekee ndo wanaweza kufanya na kusema kuwa ugumu huwa kipindi cha miaka miwili mpaka mitatu kuhudumia bila kuvuna.

Vailety Mkoma ni mkazi wa Kijiji cha Itaka wilaya ya Mbozi ameitaka jamii kuacha mila potofu na kuona kuwa mashamba ya Kahawa wanaweza kulima hata wanawake kutokana na kuwa zao hilo ni la kimkakati ambalo linaweza kumwinua kiuchumi mwanamke badala ya kubaki kulima mazao mengine tu.

“Mimi hapa mpaka sasa nina heka mbili za mashamba ya kahawa ambazo ninalima mwenyewe na ndiyo sababu hapa nimekuja na mfano wa kahawa ninayozalisha muone wanawake wenzangu tuache dhana potofu kuwa wanaume  pekee ndo wanaweza kulima zao hilo tuamke sasa ndugu zangu wanawake tunaweza na uwezo wa kulima tunao kwakuwa tuna usimamizi mzuri “amesema Mkoma.