December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia kuongoza mkutano wa Mawaziri zaidi ya 70 nchini Tanzania

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwaongoza Mawaziri zaidi ya 70 kutoka mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) kujadili masuala mbalimbali ya uchumi wa buluu ili kuweka mkakati wa pamoja kuimarisha sekta ya uvuvi.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 29, 2024 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Mawaziri wa Uvuvi, Bahari,na Maji ya Ndani kwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika, Karibiani na Pasifiki utakaofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 9-13, 2024.

Waziri Ulega amesema mkutano huo utafunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan Septemba 11 na umepangwa kufanyika sambamba na Kongamano la Kimataifa linalohusu kuhusu Mikakati ya Uboreshaji wa Mnyororo wa Uzalishaji wa Vyakula vya Majini ulioandaliwa na Serikali, kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (FAO).

“Lengo la mkutano huu unganishi, kwa maana ya Mkutano wa 8 wa Mawaziri wa OACPS, ni kujadili masuala mbalimbali ya sekta ya uvuvi katika nchi wanachama ikiwa ni pamoja na kuweka mkakati wa pamoja kuhusiana na sera zinazohusiana na masuala ya uvuvi na ufugaji viumbe maji ili kuimarisha sekta ya uvuvi katika kuchangia uchumi wa nchi wanachama,”Alisema Ulega.

Aidha Mkutano huo utatumika kama Jukwaa jumuifu litakolokutanisha watunga sera na watalaamu wetu na wenzao kutoka mataifa wanachama ili kujadili fursa na changamoto zilizopo kwenye uchumi wa buluu na hatimae kujifunza mikakati ya kutatua changamoto hizo.