Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
MADAKTARI nane kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, wanatarajiwa kutembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kwaajili ya kujifunza namna taasisi hiyo ilivyopiga hatua katika tiba ya moyo na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali kwenye vifaa tiba na wataalamu bobezi.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete JKCI, Dk Peter Kisenge amesema leo kuwa madaktari hao wanatoka katika hospitali kubwa ya rufaa ya Ngaliema iliyopo mji wa Kinshasa nchini Congo.
Alisema ujumbe wa madaktari hao utaongozwa na Dk. Kongo Minga, ambaye ni Mkurugenzi wa hospitali ya Ngaliema na kwamba ziara hiyo inatarajiwa kufanyika hapa JKCI kuanzia Jumatatu tarehe 26 hadi tarehe 31 mwezi huu.
“Hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa madaktari hawa kutoka Congo DRC kufika Tanzania kufanya ziara hii yenye dhamira ya kuzuru katika hospitali zetu kuona uwekezaji wa sekta ya afya hasa ya matibabu ya moyo uliyofanyika na serikali ya Tanzania watakuja kuona namna serikali yetu ilivyofanya mambo makubwa kwenye sekta ya afya hususan tiba ya moyo kwa kuweka mitambo ya kisasa ya tiba ya moyo,” alisema.
Alisema ziara ya madaktari hao inatokana na uwekezaji mkubwa wa serikali kwa taasisi ya JKCI ambayo ina madaktari bingwa wa kutosha wa moyo kwa watoto na watu wazima na mitambo mbalimbali ya kisasa ambayo ni kama ile iliyoko kwenye hospitali za nchi zilizoendelea ikiwemo mitambo miwili ya Cathlab.
Alisema ziara hiyo itasaidia kuendeleza uhusiano mwema kati ya Tanzania na Congo DRC katika kuboresha matibabu ya moyo ikiwa na dhamira ya kujengeana uwezo wa kimatibabu hasa matibabu ya moyo.
Aidha, alisema ziara hiyo inakuja baada ya timu ya madaktari na wawakilishi kutoka JKCI na Muhimbili kwenda nchini Congo katika ziara ya kitabibu huko Ngaliema, Kinshasa mwezi wa tano mwaka huu.
“Madaktari wa JKCI na Muhimbili walitembelea hospitali za Congo DRC na walijenga uhusiano mzuri kama taasisi za kitabibu hivyo ziara hii inayotarajiwa kuanza Jumatatu ni chachu kwa sekta yetu ya afya ikiwa Tanzania inajikita kuwa kitovu cha tiba utalii kati ya nchi za kusini mwa Sahara, “ alisema
“Tunajivunia uwekezaji mkubwa wa Serikali yetu katika vifaa tiba na rasilimali watu kuboresha huduma za Afya hivyo ujio wa madaktari hawa ni sehemu ya kutengeneza uhusiano mzuri na nchi jirani lakini pia kutangaza matibabu bora yanayopatikana Tanzania,” alisema Mollel ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Tiba utalii Taifa.
Alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyojitahidi kuwekeza vifaa vya kisasa na vya kutoka na kusomesha madaktari bingwa kwenye hospitali mbalimbali katika mikoa yote nchini.
Alisema zamani watu walikuwa wakiugua wanawaza kwenda India na mataifa mbalimbali yaliyoendelea lakini uwekezaji uliofanywa na serikali sasa watu wanatoka mataifa mbalimbali kuja kutibiwa katika hospitali za Tanzania.
“Kwa tiba ya moyo Tanzania imepiga hatua kubwa sana kwani mbali na hawa DRC wanaotarajiwa kuja wiki ijayo mataifa mengi yaliwahi kuja kujifunza namna tulivyofanikiwa kuwekeza kwenye vifaa na madaktari, wagonjwa wa moyo wa Tanzania wanatibiwa hapa hapa nchini kwasababu kile walichokuwa wakikifuata nje sasa hivi kipo JKCI,” alisema
More Stories
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja
Gavu aanika miradi iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita Geita