November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia ataja mafanikio yanayotokana na Kizimkazi

*Awataka wadau kujitokeza zaidi kushika mkono kufanikisha malengo ya Kizimkazi,
aimwagia sifa NMB kwa ufadhili ujenzi wa shule pamoja na kutambulika kimataifa

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Zanzibar

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema Tamasha la Kizimkazi limeendelea kujipambanua kuwa la kimaendeleo na chachu ya utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa wananchi

Rais Samia alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua Shule ya Maandalizi ya Tasani kwa sasa inaitwa Dk Samia Suluhu Hassan iliyopo Makunduchi mkoani wa Kusini Unguja. Shule hiyo ya kisasa imejengwa kwa ufadhili wa Benki ya NMB.

Kizimkazi ni tamasha lililoanza mwaka 2015 na lilikuwa sherehe ya kumuaga Samia baada ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais wa CCM wa hayati John Magufuli lililojulikana kama Samia Day na ilipofika mwaka 2017 lilibadilishwa jina kuwa Kizimkazi Day.

Rais Samia, alisema Tamasha la Kizimkazi litagusa kila eneo ndani ya Wilaya ya Kusini Unguja, akisema taasisi za fedha na mashirika yameonesha nia ya kuunga mkono jitihada hizo.

Aliwataka wadau kujitokeza zaidi kushika mkono kufanikisha malengo ya Kizimkazi. Kwa mujibu wa Rais Samia ana matumaini tamasha la mwaka huu visiwani Zanzibar limechochea maendeleo kwa sababu kuna miradi mingi imeanza kuzinduliwa

Alisema miradi mingine inasubiri kuzinduliwa pia. Kuhusu shule iliyojengwa na NMB, Rais Samia alisema sera ya afya na uzazi bora, inaeleza siku 1,000 baada ya mtoto kuzaliwa sawa na miaka mitatu ni muhimu, hivyo shule hiyo itakuwa kituo chao.

“Siku hizi ni muhimu kwanza mtoto apate chakula bora kitakachomjenga na afya, mwili na akili, sasa watoto watakaoletwa hapa wenye umri wa miaka miwili, mitatu na kuendelea watatunzwa na kupata makuzi ya kimwili yatakayowawezesha kuijenga akili yao kwa ajili ya masomo ya baadaye,” alisema.

. Aliwataka wazazi kuchangia matunzo ya shule hiyo ili kuendelea kuwa ubora wake akisema shule hiyo itawalea watoto kimaadili ya namna tabia za maisha zinavyotakiwa kuwa ikiwamo kula, kusalimia na kujisaidia.

“Mtoto akitoka hapa kwenda shule ya msingi anajua kila kitu kwa sababu atafunzwa maadili na kujitambua yeye ni nani, anatakiwa kufanya nini. Wosia wangu wazazi leteni watoto hapa, lakini tusaidie michango ili kuitunza shule hii,”alisema Rais Samia.

Mbali na hilo, Rais Samia aliishukuru NMB kwa kufadhili ujenzi wa shule hiyo kwa gharama ya sh. milioni 800 pamoja na miradi mingine ya maendeleo ikiwamo inayohusisha Tamasha la Kizimkazi. Pia ameipongeza NMB kwa kutambulika duniani kutokana na kujali mazingira, utawala bora na jamii.

“Hili la jamii ndilo hili, wanafanya hivi kwa sababu jamii ndiyo inayowapa uwezo, hivyo lazima warudishe hisani. Nashukuru kwa ubora wa ujenzi wa shule hii, hii ni shule ya mfano jamani katika zile zinazojengwa za maandalizi,”alisema Rais Samia.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Ruth Zaipuna alisema uzinduzi wa shule hiyo unaashiria mwanzo mzuri wa watoto wa Makunduchi kupata elimu yao katika mazingira ya awali na itakuwa msingi mzuri kwa wanafunzi wanoazunguka Kijiji cha Tasani. “Mwaka 2023 tulikutana hapa wakati unaweka jiwe la msingi na tulikuahidi tutakukabidhi shule hii kabla ya mwaka 2024, ninayo furaha kuwa ndoto imetimia na tunakukabidhi shule hii iliyopewa jina la Dk Samia Suluhu Hassan.

“Shule hii imejengwa na kuwekwa miundombinu ya kisasa ikiwamo maeneo ya kucheza ili kuwapa watoto wetu mazingira mazuri ya kujifunza pamoja na kujenga afya zao. Shule hii ina madarasa matano, kila moja linachukua wanafunzi 40,” Zaipuna.

Alisema wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi, makadirio ya ujenzi wa shule hiyo ilikuwa sh. milioni 600, lakini hadi kukamilika kwake imetumika sh. milioni 800 ikiwa ni pamoja na eneo bwalo la chakula, samani za walimu na wanafunzi na viyoyozi kwenye ofisi za walimu.

“Hii ni alama ya matumaini na ndoto mpya kwa watoto wetu watakaojengewa msingi imara wa elimu itakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye,” alisema Zaipuna.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa amezipongeza Serikali za Tanzania na Zanzibar kwa kufanya kazi kwa pamoja na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Waziri Lela alimshukuru Rais Samia kwa kuanzisha Tamasha la Kizimkazi lililojikita katika maendeleo yanayogusa maisha ya watu.

“Kisera elimu ya maandalizi Zanzibar ni ya lazima, ndiyo maana kila mwaka Serikali tunaongeza bajeti katika miundombinu ikiwamo shule za msingi ili kutoa elimu bora kwa watoto wetu,” alisema Waziri Lela.

……………………………….